By Anthony Mayunga, Mwananchi amayunga@mwananchipapers.co.tz
Serengeti. Wakati Polisi na uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Tanapa) ukisema askari wa hifadhi ya Taifa ya Ibanda-Kyerwa, Frank Mariki (30) aliyefariki muda mfupi baada ya kumfumania mpenzi wake alikuwa na shinikizo la damu, uongozi wa Hospitali Teule ya Nyerere mjini Mugumu unasema haujachunguza mwili wa askari huyo.
Taarifa ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa), Massana Mwishawa ambayo pia imesambazwa kupitia mitandao ya kijamii anasema chanzo cha kifo cha askari huyo wa intelijensia kilitokana na shinikizo la damu.
Kauli kama hiyo pia imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana Ijumaa Agosti 2, 2019.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha alipata shinikizo la damu kutokana na mapigo ya moyo kupanda baada ya tukio la fumanizi,” amesema Ndaki.
Kamanda huyo amesema polisi wanamshikilia, Angela Nelson aliyekuwa mpenzi wa Mariki pamoja Salehe Hashimu anayedaiwa kuwa ndiye mwanaume anayefumaniwa naye chumbani.
Wakati polisi na Tanapa wakihusisha kifo hicho na shinikizo la damu, Katibu wa Hospitali Teule ya Nyerere mjini Mugumu, Mboha Kazare ameiambia Mwananchi kuwa hadi jana mchana, uchunguzi wa mwili wa mwili wa Mariki ulikuwa haujafanyika.
“Ni kweli mwili umepokewa na kuhifadhiwa hapa hospitalini tangu Agosti Mosi, 2019 lakini hadi sasa haujachunguzwa kubaini chanzo cha kifo,” amesema Kazare
Tukio lilivyokuwa
Kabla ya kufikwa na mauti, Agosti 31, 2019, Mariki akishirikiana na rafiki yake (jina linahifadhiwa) aliwasili mjini Mugumu na kumwekea mtego mpenzi wake kwa kumdanganya kuwa asingefika nyumbani siku hiyo kutokana na kubanwa na kazi katika hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.
“Saa 4:00 asubuhi ya Agosti Mosi, 2019 Mariki akiongozana na rafiki yake alifika kwake na kumkuta mpenzi wake chumbani na mwanaume mwingine. Baada ya kumshambulia ‘mgoni’ wake na kumfunga pingu alitoka nje akisema anafuata silaha lakini ghafla aliishiwa nguvu na kuanguka chini,” amesema mmoja wa mashuhuda kwa sharti la kuhifadhiwa jina
“Tulimkimbiza hospitali kuokoa maisha yake lakini madaktari wakatueleza kuwa alishafariki,” ameongeza.
Alichokosema Angela
Akizungumza na Mwananchi akiwa chini ya ulinzi wa polisi, Angela amekana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Salehe, bali kijana huyo ambaye ni jirani yao alifika chumbani kwake kwa ajili ya kumchoma sindano za masaa alizoandikiwa hospitali.
“Sina uhusiano wa kimapenzi na Salehe, alifika kunichoma sindano na kwa sababu nilikuwa ninapika nilimwomba aketi kwenye kiti niepue chakula jikoni ndipo ghafla Mariki akiongozana na (rafiki wa marehemu) waliingia na kuanza kumshambulia wakitutuhumu kuwa wapenzi,” amesema Angela.
Amesema yawezekana mpenzi wake alikuwa akipewa taarifa za uongo na marafiki zake, jambo alilodai limesababisha vurugu zilizosababisha kifo chake.
No comments:
Post a Comment