Nchi za Bara la Afrika Tanzania ikiwemo zimesema wakati umefika sasa kwa Nchi zilizoendelea kuisaidia Afrika kujitegemea na kuliwezesha kutumia rasilimali zake yenyewe kwa maendeleo ya watu wake badala ya kulifanya Bara hilo kama eneo la kupata malighafi ya kuhudumia viwanda za nchi zilizoendelea.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Prof. Palamagamba John Kabudi ameyasema hayo baada ya kushiriki Mkutano wa Mawaziri wa Maandalizi ya Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Pacifico jijini Yokohama, Japan.
Ameongeza kuwa mkutano huo pamoja na mambo mengine umesisitiza umuhimu ya uwepo wa miundombinu ambayo inaunganisha Nchi za Kiafrika ili kuliwezesha bara la Afrika kuwa na miundo mbinu ya usafirishaji imara na zenye kuleta tija kwa wote.
Aidha Prof. Kabudi ameongeza kuwa ni mkutano huo pia umeazimia kuzitaka nchi zilizoendelea kuongeza fedha zaidi kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii hususani katika nyanja za afya hususani katika kupambana na malaria,kifua kikuu na ukimwi sambamba na Afrika kuwajibika kuchukiua hatua zote za kuhakikisha uwepo wa utawala bora,usalama na Amani.
Akifungungua mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. Kono Taro amezipongeza nchi za Afrika kwa kupiga hatua katika maendeleo kupitia ushirikiano na Japan na kwamba nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na nchi hizo ili kuziwezesha kufikia malengo ikiwemo mapinduzi ya viwanda.
Mhe. Taro amesema kuwa, ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia mpango wa TICAD umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 1993 na kwamba ni matarajio yake Mktano wa Saba utakuwa wa tija zaidi kwa pande hizo mbili.
“Nawakaribisha Mawaziri wenzangu Yokohama ambapo maandalizi ya mkutano wa saba wa kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika yanaendelea. Jukumu letu ni kupitia na kupitisha rasimu ya Azimio la Yokohama na Mpango kazi wake ili hatimaye litunufaishe sote pale litakapopitishwa na Wakuu wa nchi” alisema Mhe. Taro.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano huo, Mhe. Sameh Shoukry ameipongeza Japan kwa kuendelea kuandaa mikutano hiyo ambayo ina nia ya kuifikisha Afrika katika mapinduzi ya viwanda na kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana na nyingine nyingi.
Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Kamishenii ya Umoja wa Afrika ambao ni miongoni mwa waandaaji wenza wa Mkutano wa Saba wa TICAD, Bw. Kwesi Quartey amesema kuwa, mkutano huo unafanyika wakati Umoja wa Afrika unaendelea kutekeleza agenda 2063. Agenda hiyo pamoja na mambo mengine inalenga kuziwezesha nchi za Afrika kufikia maendeleo ya hali ya juu kwenye sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, teknolojia na miundombinu.
Kadhalika Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma za Kanda ya Afrika kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika, Bw. Lamin Manneh alisema kuwa ushirikiano kati ya Afrika na Japan kupitia TICAD umekuwa na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Bara la Afrika.
Mkutano wa Saba pamoja na mambo mengine unatoa fursa ya kupanga mikakati ya ushirikiano na agenda za kimaendeleo zitakazotelezwa kati ya Japan na Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuanzia mwaka 2019 hadi 2021.
Agenda za mkutano wa mwaka huu zinalenga kujadili mageuzi ya kiuchumi na kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kukuza sekta na uvumbuzi. Pia kuimarisha usalama na ustahimilivu endelevu kwenye jamii pamoja na kuendeleza jitihada za kuimarisha amani na usalama barani Afrika. Agenda za Mkutano wa Saba zinaenda sambamba na agenda 2063 ya Umoja wa Afrika, Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine ya kimataifa kama Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa.
Mkutano huu ambao umewashirikisha Mawaziri kutoka nchi za Afrika, na wadau mbalimbali wa maendeleo unafanyika ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utakaofanyika kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019.
No comments:
Post a Comment