Dar es Salaam. Beki wa kitaifa wa Tanzania, Abdallah Shaibu 'Ninja' ameanza mazoezi ya gym baada ya kuonyeshwa viwanja vya mazoezi na mechi na baadhi ya maeneo muhimu katika klabu yake mpya ya LA Galaxy, Marekani.
Ninja atacheza LA Galaxy kwa mkopo wa mwaka mmoja baada ya kusaini mkataba wa miaka minne kwenye timu ya MFK Vyskov ya Jamhuri ya Czech, akitokea Yanga ambako alicheza kwa misimu miwili.
Ninja ameliambia Mwanaspoti Online tayari amefanyiwa vipimo vya afya amekutwa safi ndipo alipopangiwa programu ya kufanya mazoezi ya gym asubuhi.
Kabla ya vipimo hivyo ameeleza jinsi ambavyo amepokelewa vizuri, akikiri hakutarajia katika maisha yake na hilo linampa moyo wa kupambana zaidi kufanya mambo makubwa katika soka.
"Mapokezi yalikuwa makubwa sikutegemea katika maisha yangu, kubwa nawaomba Watanzania wote kuniombea ili niweze kupeperusha bendera ya Tanzania vyema kwa kuonyesha kiwango cha juu.
"Kipekee niwashukuru Yanga ambao wameniunga mkono mwanzo wa safari mpaka nilipofika hapa, jambo ambalo litabakia kuwa kumbukumbu kwangu katika maisha ya soka,"alisema Ninja.
Yanga ilimsajili Ninja kutoka Taifa Jang'ombe ya Zanzibar, mwaka 2017 ametumika misimu miwili baada ya kumaliza mkataba wake na kutimkia Marekani.
Ninja sasa anaungana na Mtanzania mwingine chipukizi Ally Ng’anzi anayecheza kwa mkopo klabu ya Forward Madison FC ya USL League One, akitokea Minnesota United FC inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (MLS).
No comments:
Post a Comment