ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 29, 2019

Mrembo Bongo Mwenye Ukimwi Ashitua!



UKIKUTANA na mrembo Doreen Odemba, akakuambia anaishi na virusi vya Ukimwi unaweza kukataa mpaka pale atakapoamua kukuonyesha cheti chake, lakini ndiyo ukweli, mrembo huyo ni mwathirika.

Uamuzi wa Doreen, msichana mrembo na jasiri kujitangaza kuhusu afya yake, umeibua mshtuko wa aina yake kwa watu wa kada mbalimbali katika mitandao ya kijamii. Doreen, mwenyewe ameshuhudia kuishi na virusi vya Ukimwi kwa zaidi ya miaka 15 sasa, akieleza kuwa siri kuu ya afya njema aliyonayo ni kuitambua afya yake mapema, kujikubali na kuishi kwa kufuata masharti rafiki anayotakiwa kufuata mtu anayeishi na virusi hivyo.
MSHUTUKO
Mbali na gazeti hili, Doreen alipata kufanya mahojiano na Global TV na ‘clip’ ya video yake inayomwenyesha akitoa ushuhuda wake kusambaa kwa kasi kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua mshtuko.

Mtoa maoni mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Masanduki aliandika: “Kwa mtindo huu kweli kuna kupona Ukimwi kweli? Mimi kuanzia leo nafunga zipu yangu. Kumbe uzuri siyo tija. Lakini nampongeza sana dada Doreen kwa kuamua kujiweka wazi afya yake na kutoa elimu kuhusu Ukimwi.”


Sizy Lucas aliandika: “Mungu azidi kukulinda dada Doreen. Umenihamasisha sana. Mimi nakuahidi kukuunga mkono kwa kujitunza na kutofanya ngono isiyo salama. Wewe ni mpambanaji sana.” Maoni ni mengi kuhusu afya ya Doreen, huku wengine wakipinga katakata kuhusu mrembo huyo kuwa mwathirika.
MAHOJIANO MAALUM NA UWAZI
Akizungumza na Uwazi katika mahojiano maalum, Doreen alianza kwa kusimulia namna alivyoambukizwa virusi hivyo. “Nilipata maambukizi kutoka kwa wazazi wangu, lakini sikujua mpaka nilipofikisha miaka 11; wakati huo mama alikuwa amefariki, nakumbuka ilikuwa mwaka 2004.
“Awali sikujua kama nina tatizo, japo kuna watu baadhi mtaani kwetu walikuwa wanajua lakini ilikuwa ngumu kuniambia. Nilianza kuumwa kila mara, homa zisizoisha na hata nywele zangu zilianza kunyonyoka,” alisema Doreen.
ALIVYOPOKEA MAJIBU KUWA AMEATHIRIKA
Mrembo huyo alisema kuwa baada ya kupelekwa hospitali na shangazi ya na kupimwa aligundulika kuwa ana maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kitu ambacho kilimchanganya sana japo alikuwa mdogo.
“Haikuwa kazi rahisi kabisa kupokea majibu hayo, nilikuwa mdogo lakini kwa kweli nilichanganyikiwa ila nashukuru sana hospitali walijaribu sana kuwa nami kwa ushauri wa karibu nikaanza kupata moyo na kukubali hali yangu.”
AWAPASULIA RAFIKI ZAKE TATIZO LAKE
Doreen aliendelea kusema kuwa kwa sababu aliipokea hiyo hali, hakuwa na jinsi ilibidi awaambie ukweli rafiki zake ambapo wengi wao waliona huruma na wakazidi kuwa naye karibu na marafiki wengine kuongezeka. “Niliamua kufanya hivyo ili kila mtu aliye karibu nami ajue nini kipo kwangu, lakini nashukuru walinipa mapenzi na hata kuongeza marafiki wengine wengi,” alisema.
KWA NINI ALIAMUA KUJITANGAZA?
Doreen anasema aliona ni vizuri kuokoa kizazi kijacho na kuwaonyesha kuwa kufanya hivyo kunaweza kukufanya kuishi muda mrefu kwa matumaini. “Nilitaka watu wajue
kupata maambukizi sio jambo la kushangaza maana ni ugonjwa kama yalivyo magonjwa mengine. Tangu nimeamua kujiweka wazi, niko na amani kubwa sana moyoni kwa sababu najua kabisa nawaelimisha maelfu ya vijana wengi na kuokoa maisha yao,” alisema na kuongeza:
“Wanaume wengi wananisumbua, wananitaka bila kujua kuwa naishi na Ukimwi. Siku zote nimekuwa mkweli kwao, wanaoleta ubishi nawaonyesha cheti, wanaishia kushtuka na kuondoka zao, hapo najua hakuwa na penzi la kweli kwangu.”
ANA MPENZI?
“Nilikuwa naye lakini tumeshaachana, kwa sasa sina. Mpenzi wangu huyo yeye hakuwa na maambukizi na haikuwa shida kwetu kwa sababu nilimwambia kabla, tukaenda kupima na kuthibitika kuwa mimi nilikuwa nao, yeye alikuwa sawa. “Tulidumu kwa miaka zaidi ya miwili lakini tulishindwana, baadhi ya mambo hatukuendana. Mpaka sasa bado sijapata mpenzi mwingine,” alisema.
ANA NDOTO YA KUWA NA FAMILIA YAKE
Doreen anasema ana ndoto ya kuwa mama mwenye familia ya mume na watoto, hivyo anaomba Mungu ampe mume mwema wa kukamilisha ndoto yake hiyo. “Kikubwa sana nina ndoto ya kuwa na familia yangu, ndiyo kitu kikubwa ninachomuomba Mungu siku zote,” alisema.
AWAASA MASTAA
“Najua kuna mastaa wapo katika hali kama yangu, lakini wanafanya siri. Wajitangaze ili watu wajue na kama mtu akimpenda, ajue kuwa yupo kwenye hali gani. Isiwe kama unamkomoa mwenzako.
“Kuwa na Ukimwi siyo kufa, pia mtu asiye na maambukizi anaweza kuishi na mtu mwenye maambukizi, kuna elimu ya kuishi na mtu mwenye Ukimwi, ndiyo maana mimi sina hofu. Mtu akinipenda, namweleza ukweli asipoamini namwonyesha vyeti, kama ananipenda kweli atabaki lakini kama alikuwa anapita ataenda,” alimalizia Doreen katika mahojiano haya maalum.
KUTOKA MHARIRI
Tunampongeza Doreen kwa uamuzi wake wa kujitangaza afya yake, lakini kutoa elimu kwa umma na hasa vijana kuhusu maambukizi ya Ukimwi.
Kupitia Doreen, naamini Watanzania watakuwa wamejifunza kitu muhimu kuhusu Ukimwi na kuchukua tahadhari, kwani huwezi kutambua mwathirika kwa kumtazama kwa macho. GPL

No comments: