Wakati wa shambulio la Albino nchini,nilimwuliza mwanasiasa mmoja kama chama chake kinacho sera ya kupambana na tatizo la ushirikina. Akanijibu, “ hapana”. Alafu kwa mshangao mkubwa, akaendelea kusema kuwa ushirikina ni tatizo dogo sana nchini na unafanywa na watu wachache, wengi wao ni wazee na watu wasio na elimu. “Dawa ya ushirikina ni kugeuza kichwa mpaka imani yake ipotee.”
Jibu la huyu mwanasiasa limekuwa likinirudia kila wakati nikiwa naangalia matatizo ya kisiasa ulimwenguni. Kwa mfano, Wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2016, chama cha Democrati, kiligeuzia kichwa tatizo la rangi Marekani ,lakini tofauti ni kuwa, tatizo halikufutika , na limekuwa moja ya mambo makubwa yanayoikabiri siasa ya nchi mbele ya uchaguzi mkuu mwakani.
Kwanza ni lazima niweke wazi kuwa nia yangu hapa ni kufananisha matatizo mawili, tatizo la rangi la Marekani na tatizo la ushirikina nchini. Na kama kuna mtu anaamini kuwa wazungu au washabiki wote wa Trump ni wabaguzi wa rangi, basi inabidi aende hospitali ya Mirembe.
Kama Tanzania ilivyo na tatizo la ushirikina, Marekani wanalo tatizo la rangi. Ubaguzi wa rangi nchini Marekani ulianza toka karne ya 17, wakati wa biashara ya watumwa. Siashara ya utumwa ulipopigwa marufuku mwaka 1860, na baada ya vita vya ndani ya nchi vya mwaka 1863, Marekani ikapitisha sheria ya kufungulia ubaguzi wa watu weusi iliyojulikana kama, Jim Crow. Sheria za Jim Crow zilizuia watu weusi wasichanganyike na Wazungu kwenye mahospitali,migahawa, kwenye vyombo vya usafirishaji , mahotelini , mpaka kwenye ndoa.
Mwaka 1948, karibu karne moja baada ya Jim Crow, watu weusi wakapata ushindi wa kwanza wa mahakama kuu wa kusitisha sheria za kibaguzi. Kwenye kesi ya Brown v Board of education, mahakama kuu iliamua kuwa katiba ya nchi inakataza ubaguzi wa rangi kwenye shule za serikali. Na baada ya hapo, watu weusi waliendelea kurudishiwa haki zao nyingi kupitia mahakamani na bungeni. Mwaka 1967, voting rights ikapitishwa na bunge, watu weusi wakaruhusiwa kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu. Ingawaje ongezeko la haki za weusi ilichukuliwa kama hatua kubwa ya maendeleo nchini, baadhi ya wazungu walichukulia kama ni mashambulizi ya rangi yao.
Kama ilivyo Tanzania na tatizo la washirikina , wabaguzi wengi wa Marekani wanaishi kwenye miji midogo na vijijini.Na pia kama washirikina wa Tanzania walivyoamini kuwa viungo vya Albino vinaleta utajiri. Wabaguzi wa Marekani wanaamini kuwa kama watazidiwa idadi na watu wa rangi nyingine, watu weusi watalipiza kisasi kwa kuwafanya wawe watumwa. Na wengine wanaamini kuwa, wakizidiwa idadi, watapoteza, umuhimu wao kwanye sekta za uchumi, mashuleni, kazi, na serikarini.
Labda watu wengi wanaweza kuona hizi hofu za wazungu ni kichekesho , lakini sehemu kadhaa ya wazungu wanaamini hivyo na pia ni makosa makubwa kudharau kabisa dukuduku lao. Dukuduku kama ukweli kuwa idadi ya wazungu inapungua kwa kasi kubwa Marekani . Mwaka 1963, kwa mfano, wakati raisi Kennedy alipopitisha sera ya kufungulia uhamiaji wa watu wasio wazungu kuja Marekani, idadi ya Wazungu ilikuwa ni 90%, mwaka 1975, idadi ya Wazungu ikashuka kuwa 80%, na sasa hivi ni 65%. Na kufanya mambo yawe yanatisha zaidi , makadirio ya sensa yanaonyesha kuwa ikifika mwaka 2050, idadi ya wazungu itashuka kuwa chini ya 50%.
Ingawaje yule mwanasiasa niliyeonana naye ,chama chake kilishinda uchaguzi uliofuatia, na washirikina toka baada ya janga la Albino, hawajaliweka taifa letu tena kwenye ukurasa wa mbele wa magarazeti ya kimataifa, siasa za Marekani zimekuwa ni gumzo la kila siku kwenye magazeti duniani. Wazungu wengi waliompigia kura za uraisi Obama na Demokrati kwenye uchaguzi wa mwaka 2008 na 2012, waligeuza kura zao na kumpigia Trump kwemye uchaguzi wa uraisi 2016.
Trump analielewa hili tatizo la rangi nchini , na anajua jinsi ya kulichombeza. Kama chama cha Democrati kitaendelea kuligeuzia kichwa tatizo la rangi nchini, na pia kama hakito weka sera halisi za kudhibiti mipaka ya nchi na uhamiaji usiofuata sheria kwenye mpaka wa kusini, Trump ataendelea kupiga vuvuzela lake la rangi, na wabaguzi wengi watalifuata wacheze nae. Na wale Wazungu wengine wasio wabaguzi lakini wanaohofia kuwa rangi yao ipo hatarini kupotea , watajiunga naye, na hatimaye, atashinda uchaguzi mara nyingine.
No comments:
Post a Comment