ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 31, 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Akutana Na Waziri Mkuu Wa Japan, Rais Wa JICA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe na kuishukuru Serikali ya Japan kwa ushirikiano inaoutoa kwa Tanzania.

Amekutana na kiongozi huyo leo (Jumamosi, Agosti 31, 2019) katika hoteli ya The New Otani, Tokyo Japan. Amesema Tanzania inaheshimu uhusiano mzuri uliopo kati yake na Japan

Mazungumzo yao yalihusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kidiplomasia pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa kwa ushirikiano kati ya Japan na nchi yetu.

Waziri Mkuu ameishukuru Japan kwa misaada mbalimbali ya maendeleo inayoitoa nchini ambayo imesaidia katika kujenga uchumi na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji hususan wenye viwanda wawekeze nchini ili washirikiane na Watanzania kukuza uchumi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kukuza uchumi na kufikia wa kati ifikapo 2025 kupitia sekta ya viwanda.

“Japan imepiga hatua kubwa katika tekinolojia hivyo naamini kuwa  wafanyabiashara na wenye viwanda  kutoka Japan wakiwekeza Tanzania wataleta tekinolojia yao pia.”

Awali, Waziri Mkuu alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Shinichi Kitaoka.

Katika mazungumzo hayo kiongozi huyo wa JICA alisema wameridhia kuwa wataendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutia saini mikataba mbalimbali yenye lengo kuinua maisha ya watanzania na kujenga uchumi.

Waziri Mkuu aliishukuru JICA kwa ushirikiano unaoutoa nchini likiwemo suala la kuendelea kuwapokea wanafunzi wa Kitanzania na kuwasomesha katika taaluma mbalimbali. Amesema Tanzania inathamini sana mchango unaotolewa na JICA katika ujenzi wa barabara, huduma za Afya na elimu.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,        
JUMAMOSI, AGOSTI 31, 2019.

No comments: