ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 3, 2019

Waziri wa Afya afanya ziara Hospitali ya Kivunge kuzungumza na watendaji

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akitoa taarifa kwa Wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja kuhusu utaratibu wa kuingia kazini (shifti) kwa Wafanyakazi wa hospitali hiyo.
Mkurugenzi Utumishi Wizara ya Afya Ramadhan Khamis Juma akizungumza na Wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja juu ya kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa ufanisi,kushoto ni Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed.
Mkurugenzi Tiba kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja Dkt. Juma Salum Mbwana akiwahimiza Wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja kufanya kazi zao inavyotakiwa (kulia) - Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini “A” Unguja wakifatilia kwa makini maelezo ya Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed huko katika Hospitali hiyo.
Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.


Na Mwashungi Tahir Maelezo 2-08-2019.
WAZIRI wa Afya Hamad Rashid Mohamed amewaagiza Viongozi na Wafanyakazi wa Hospitali ya Kivunge kuingia kazini kwa zamu (Shifti) kama ilivyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja ili wananchi waweze kupatiwa huduma muda wote wanapozihitaji.
Amesema agizo hilo linapaswa kutekelezwa ifikapo Jumaatatu wiki ijayo ili kuhakikisha Afya za wananchi zinaimarishwa kwa kupatiwa matibabu muda muafaka.
Wito huo ameutoa katika Hospital ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini A, kuhusu malalamiko yanayotolewa na Wananchi kwa kukosa huduma kwa wakati.
Amesema utaratibu wa Shifti utaondosha malalamiko yaliyojitokeza na itaweza kutambulikana kila mfanyakazi utendaji wake wa kazi.
Aidha amesema utaratibu wa Shifti utasaidia pia kutekeleza kanuni na sheria za uajiri kwa mpango maalum unaotakiwa.
“Huu ni mpango rasmi wa Serikali utakaoanza wiki ijayo tunaanza kwa Hospitali ya Kivunge, utakwenda na Makunduchi na nyengine zinafuatia,”alisema Waziri Hamad.
Aidha alisema Hospital ya Kivunge ni ya Wilaya ambayo imetangazwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Ali Mohamed Shein hivyo wafanyakazi wanapaswa kuwajibika kikamilifu ili kukidhi haja ya Wananchi.
Waziri Hamad amewataka Wafanyakazi hao kutumia lugha nzuri katika kuwahudumia wagonjwa kwani lugha nzuri huwapa faraja na kuwajengea sifa hata Madaktari wanaotoa huduma.
Aidha amewakumbusha wafanyakazi kuheshimu majukumu yao na sheria ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kuchelewa kazini na kufika mapema ili huduma zipatikane kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Utumishi wa Wizara ya Afya Ramadhani Khamis Juma alisema kwa upande wa utumishi Serikali imejitahidi kuwasomesha ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati.
Hivyo amewaasa wafanyakazi waache kujipangia wenyewe kufanya kazi kwani Sheria ya utumishi inamtaka mfanyakazi afanye kazi kwa masaa manane na siyo kama wanavyotaka wao.

Kwa upande wa Mkurugenzi tiba wa Hospitali ya Mnazi Mmoja Dr Juma Salum Mbwana aliwataka kujirekebisha na kufanya kazi kwa bidii na kuepukana na kuwajibishwa kwa barua au onyo kwani kunaharibu utendaji wako wa kazi.

No comments: