Jeshi la Polisi mkoani Iringa, limesema kuwa limebaini tukio lililotokea la mchawi kudondoka juu ya paa la nyumba ya Mchungaji eneo la Ilula ni la kutengenezwa, mwanamke huyo alilipwa pesa ili kutengeneza sakata hilo.
Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Juma Bwile amesema kuwa mama huyo ambaye amejitambulisha kwa jina la Bi. Kabula Masunga hapo awali alidanganya kwamba jina lake kamili ni Magreth Simon ili kukwepa ukweli.
Amesema awali Bi. Magreth Simon alisema kuwa anatokea Morogoro lakini ni mkazi wa Sengerema Mkoani Mwanza kama ambavyo amebainisha mumewe Bw. Jeremia Yustas, baada ya kutoa taarifa Makao Makuu ya Polisi Mkoani Iringa.
Aidha mumewe Bw. Jeremiah Yustas amesema Bi. Kabula aliaga kuwa anaelekea Musoma kwa ajili ya kujengea makaburi ya ndugu zake na kwamba anashangaa kuona ameshikwa mkoani Iringa kwa uchawi.
Nao wakazi wa mji mdogo wa Ilula wamesema kitendo hicho hakivumiliki, hivyo basi wananchi wanatakiwa kuwa makini kwakuwa mama huyo angeweza kuuawa na wananchi ambao wanaamini ushirikina.
Mapema mwezi Agosti, Jeshi la Polisi mkoani Iringa lilimkamata mama huyo ajulikanaye kwa jina la Kabula Masunga akiwa amelala juu ya paa la nyumba ya Mchungaji Jeremiah Charles katika halmashauri ya Mji Mdogo wa Ilula, Wilayani Kilolo, mkoani Iringa baada ya wananchi kumtuhumu kuwa ni mchawi.
No comments:
Post a Comment