ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 30, 2019

JIANDAENI NA MAISHA YA UZEENI ILI MSIJE KUILALAMIKIA SERIKALI – RC MTWARA

 Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa akiongea na mzee aliyefika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona kupata matibabu bure ya wazee kabla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayoendelea Mkoani Mtwara.
 Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa akisoma bango katika viwanja vya Nangwanda Sijaona kabla ya kufungua Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayoendelea Mkoani Mtwara.
  Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiongea na vyombo vya habari mara baada ya ufunguzi  Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayoendelea Mkoani Mtwara.
Baadhi ya wazee wakiendelea kupatiwa huduma ya matibabu bure wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yanayoendelea Mkoani Mtwara.


Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa amewataka vijana ambao bado wana nguvu za kufanya kazi kujiandaa vyema na maisha ya uzeeni ili kuepuka kutoa lawama na kulalamikia Serikali katika maisha yao ya uzeeni.

Aidha Kiongozi huyo nameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutunga Sheria ambayo itaainisha majukumu ya watoto kwa wazee, majukumu ya wazee kwa watoto pamoja na majukumu ya Serikali kwa wazee ikiwemo haki ya kulinda wazee kama ilivyo sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Byakanwa  amesema hayo leo wakati wa akizindua Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Wazee Duniani yanayoadhimishwa Kitaifa Mkoani Mtwara  kwa Siku tatu kuanzia Septemba 29, na kufikia kiklele chake Octoba 1, 2019.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara aliongeza kuwa wakati wa utunzi wa sheria ya wazee majukumu mengi yasirundikwe kwa Serikali lakini sheria hiyo iyaangazie majukumu hayo kwa jamii ili ione umuhimu wa kuwa na wajibu wa kuwatunza wazee.
 Byakanwa pia ametoa angalizo kwa viongozi walio Serikalini sasa kutambua kuwa suala hili sio la wazee peke yao bali ni suala lao  pia hivyo ni vyema wakatumia fursa waliyonayo  kuweka mazingira mazuri kwa wazee ili nao wafaidike nayo wakati wa uzee wao.

Aidha  Byakanwa amewataka vijana ambao kwa sasa  wananguvu kujiandaa kwa ajili ya uzee ili muda wao wa uzee wautumie vizuri kwa kukaa na kukumbushana masuala ambayo yatawapa faraja lakini sio kufikiria kuanza kuwekeza mitaji katika biashara.

Kiongozi huyo wa Mkoa wa Mtwara ameongeza kuwa ukatili dhidi ya wazee uko zaidi kwa jamii na sio ndani ya serikali na kwa kiasi kikubwa unafanywa kwa wazee ambao walitumia nguvu kubwa kuwatunza na kuwalea wakiwa watoto.

"Hili linalowatokea wazee ni fundisho kwa wengi kwamba sio lazima unapomtunza mtoto naye atakuja kukutunza kwasababu wazee wengi wako peke yao maana watoto wao wako sehemu mbalimbali wakitafuta maisha na wengine wamesahau kama wazee waliwalea na kuwatunza’’. Aliongeza Byakanwa.     

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu katika hotuba yake kwa Mgeni rasmi amesema kuwa changamoto zinazowakabili hapa Nchini ni pamoja na umasikini uanaotokana na ukosefu wa nguvu za kufanya kazi pamoja na magonjwa yanayotoka na umri kuwa mkubwa.

Aidha Dkt Jingu ameongeza kuwa changamoto nyingine inatokana na watu kushindwa kujiandaa na maisha ya uzee lakini pia akiongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha inatoa huduma kwa wazee ili kuweza kupunguza changamoto zinazowakabili.

Dkt. Jingu ametaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na Sera ya matibabu bure kwa wazee, uwepo wa mabaraza ya wazee na mapitio ya Sera ya wazee ili kuhakikisha kuwa inajitosheleza lakini pia Serikali ina makao 17 ya wazee ambayo yanapokea wazee wasiokuwa na ndugu wala Jamii ya kuwahudumia.

No comments: