Serikali imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2019 kwa lengo la kurekebisha sheria 11.
Sheria zinazopendekezwa kufumuliwa ni pamoja na Sheria ya Mapato Yatokanayo na Uhalifu, Sura ya 256 kwa lengo la kuipa mahakama uwezo wa kutaifisha mali tofauti na iliyopatikana kwa uhalifu endapo itagundulika upatikanaji wake si halali, kufichwa au kutoroshwa nje ya nchi.
Katika marekebisho hayo, pia inapendekezwa uwapo wa kifungu kipya cha 14B kitakachoipa mahakama uwezo wa kuzuia uhamisho wowote wa mali ambao umefanyika kwa lengo la kukwepesha mali kutaifishwa.
Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma jana muswada huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Adelardus Kilangi, alisema marekebisho hayo yanalenga wahalifu kutonufaika na mali zozote zitokanazo na makosa ya rushwa, usafirishaji dawa za kulevya, utakatishaji fedha na makosa mengine yanayohusiana.
Alisema kabla ya maombi ya kutaifisha hayajafanywa au ndani ya miaka mitano kuanzia siku ya mwisho ya tukio kutokea, mali hiyo itahesabiwa ni zao la uhalifu.
Prof. Kilangi alisema mapendekezo katika kifungu cha 38 yanalenga kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka kuwasilisha mahakamani maombi ya upande mmoja ya kuzuia mali pale ambapo mhusika anachunguzwa au hawezi kufika mahakamani au alishahukumiwa kwa kosa linalohusiana na mali iliyotaifishwa.
"Kifungu cha 56 kinapendekezwa kufutwa kwa lengo la kuondoa mahitaji yasiyo ya lazima dhidi ya serikali ya kulipa gharama za madhara yanayotokana na amri ya zuio iliyowekwa," Prof. Kilangi alisema.
Katika muswada huo, serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ili kuwazuia maofisa sheria au mawakili wa serikali na wanasheria walioko kwenye utumishi wa umma, kufanya kazi za uwakili wa kujitegemea isipokuwa kushuhudia viapo na uhakiki wa nyaraka.
"Mawakili wa serikali wanaweza tu kufanyakazi za uwakili wa kujitegemea kwa kibali maalum cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa sababu maalum.
"Wanasheria wanaokusudiwa ni wanasheria wote katika utumishi wa umma ambao wanaongozwa na Kanuni za Maadili ya Wanasheria katika Utumishi wa Umma," alisema.
Katika muswada huo, serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo, Sura ya 108, kwa lengo la kupanua wigo wa mfumo wa usajili wa vizazi na vifo vikijumuisha vifo vinavyotokea nje ya nchi.
Prof. Kilangi alisema marekebisho hayo pia yanalenga kuwatambua watendaji wa kata na vijiji kama wasajili wasaidizi baada ya kukasimiwa mamlaka hayo na Msajili Mkuu.
Alisema muswada huo pia unalenga kufanya marekebisho katika Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20, ili kuwe na makubaliano kati ya Mwendesha Mashtaka na mtuhumiwa au wakili wake, kupunguza uzito wa adhabu pale ambapo mtuhumiwa atakiri kosa analoshitakiwa nalo.
Alisema utaratibu huo utasaidia kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kupunguza msongomano wa wafungwa magerezani.
Prof. Kilangi pia alisema serikali inapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Urejeshaji Wahalifu, Sura ya 368, kwa lengo la kuboresha utaratibu wa kisheria wa ushirikiano wa kimataifa katika kusaidiana kurejesha watuhumiwa katika kesi za jinai.
Alisema muswada huo pia unalenga kufanya marekebisho katika Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11, kwa lengo la kuongeza kiwango cha thamani ya kifedha katika mashauri ya madai yanayosikilizwa katika mahakama hizo kutoka Sh. milioni 50 cha sasa hadi Sh. milioni 100.
Kilangi pia alisema muswada huo unalenga kufanya marekebisho katika Sheria ya Chama cha Msalaba Mwekundu Tanganyika, Sura ya 66, ili itumike pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupanua wigo wa majukumu ya chama hicho kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment