ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 6, 2019

Mgogoro Kati Ya Wafugaji Na Wakaulima Kijiji Kashanda Wilayani Karagwe Sasa Kupatiwa Mwarobaini Wake

Na Avitus  Benedicto Kyaruzi, Kagera
Mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu zaidi ya miaka kumi na kusababisha uvunjifu wa amani kati ya pande mbili za wananchi ambao ni  wakulima na wafugaji katika Kijiji cha Kashanda Kata Bugene Wilayani Karagwe sasa utapatiwa ufumbuzi wa kudumu mara baada ya Mkuu wa Mkoa kuingilia kati ili kurejesha amani ya kudumu katika eneo hilo.
 
Baada ya kuwa anapokea malalamiko mengi kwa muda mrefu kuhusu Kijiji Kashanda Mkuu wa Mkoa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti aliamua kufika eneo la kijiji hicho cha Kashanda Septemba 4, 2019 pamoja na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ili kujionea mwenyewe jinsi mgogoro ulivyo  ili uweze kuutolewa maamuzi sahihi.
 
Mhe. Gaguti alipofika katika eneo hilo la Kashanda alikuta ni eneo ambalo halina wananchi ambao wanaishi kama kijiji bali aliwakuta baadhi ya vijana kutoka Wilayani Ngara wakiwa wanafyeka miti na vichaka wakiendelea kulima katika maeneo mbalimbali wakidai kuwa nao wameajiriwa kulima na wamiliki wa maeneo hayo.
 
Aidha, Mkuu wa Mkoa Gaguti hakukuta mifugo ya aina yoyote ile katika eneo hilo bali baadhi ya wakulima ambao walikuwa wamefyeka miti na vichaka ndani ya eneo hilo wakiendelea kulima kwa ajili ya msimu wa kupanda maharage na mahindi na mazao mengiyo.

Kwa maelezo kutoka katika uongozi wa Wilaya ya Karagwe wakiuelezea mgogoro huo walimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa baada ya kutokea uvunjifu  wa amani mara kwa mara wakulima wakijihami na siraha za jadi kama mapanga, mikuki na upinde na wakiwashambulia wafugaji, wafugaji waliamua kuondoa mifugo yao katika eneo hilo ambalo walitengewa kwa kwaajili ya kulishia mifugo yao hasa ng’ombe.
 
Mkuu wa Mkoa Gaguti baada ya kutembelea eneo la kijiji hicho cha Kashanda na kuona hali halisi alisema kuwa amelielewa eneo lenyewe la mgogoro, pili ndani ya muda mfupi sana ataitisha kikao cha pamoja uongozi wa kijiji hicho cha Kashanda, uongozi wa Wilaya ya Karagwe pamoja na wataalam wote wa ardhi wanaohusika na atatoa maamuzi yenye maslahi mapana ya wananchi, Wilaya na Taifa kwa ujumla.
 
Kijiji cha Kashanda kipo Kata Nyakahanga Tarafa Bugene Wilayani Karagwe na kina hekta za mraba 3,370.319 na kiliandikishwa kwa hati namba KAG/KIJ 507 chini ya kifungu namba 22 cha sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya mwaka 1982 na hati hiyo ilitolewa tarehe 23 Mei, 1989.
 
Pamoja na kijiji cha Kashanda kuandiskishwa na kusajiliwa na Serikali hakikutajwa kama kijiji cha wafugaji bali kinatajwa kama vijiji vinginevyo vilivyosajiliwa na Serikali. Aidha, kwa maelezo ya wananchi wa eneo hilo pamoja na Wilaya ni kwamba kijiji Kashanda kilianzishwa kwa kumega maeneo ya vijiji vya Bishehe, Omulusimbi, Chonyonyo na Chabalisa ili wafugaji wapate sehemu ya kulishia mifugo yao lakini baadae eneo hilo lilianza kuvamiwa na wakulima.
 
Kutokana na mgogogo huo kusababisa uvunjifu wa amani wa mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima wanaolivamia eneo hilo Mkuu wa Mkoa Gaguti amesema kuwa sasa basi lazima mgogoro huo ufike mwisho na ijulikane wazi ni shughuli zipi zinatakiwa kuendelea kufanyika katika eneo hilo ufugaji au kilimo. 

“Nataka Mkoa wa Kagera migogoro ya ardhi ikomeshwe kabisha na uwe mkoa wa mfano.” Alimaliza kwa kusisitiza Mhe. Gaguti

No comments: