Na Shamimu Nyaki –WHUSM
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza amesema kuwa Serikali haishikizi ufadhili katika michezo bali wajibu wake ni kuweka mazingira wezeshi kwa mfadhili ambaye anataka kufadhili mchezo wowote kutokana na yeye kuona namna anavyoweza kufaidika katika ufadhili huo.
Mhe.Shonza amesema hayo leo Bungeni Dodoma alipokuwa anajibu swali la Mbunge Mhe.Sophia Mwakagenda (Viti Maalum) aliyeuliza Ni lini Serikali itahakikisha ufadhili unapatikana kwenye michezo inayohusu wanawake hususan michezo ya ngumi.
Akijibu swali hilo Mhe.Shonza ameeleza kuwa ufadhili wa michezo hutokana na mfadhili kuona faida ya kibiashara na kijamii wakati anapofadhili ambapo amesititiza kuwa hivi sasa Tanzania ina ligi kuu ya mpira wa miguu kwa wanawake ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya vinywaji ya Serengeti Breweries kupitia bia yake ya Serengeti Lite ambayo imefadhili kutokana na faida walioona itapata.
“Ufadhili haushinikizwi na Serikali bali ni suala la hiari kwa upande wa wafadhili ambao huchukua fursa hiyo pale wamapoona fursa za kibiashara zitakazowanufaisha wao, Hivyo wajibu wa Serikali ni kuimarisha uhusiano na kuweka mazingira wezeshi ili faida ipatikane kwa pande zote mbili”alisisitiza Mhe.Shonza.
Aidha Mhe. Shonza katika kujibu swali la nyongeza la mbunge huyo aliyeuliza ni lini Serikali itatoa vifa vya mazoezi kwa wanamichezo hao, ameeleza kuwa suala la kukuza na kuendeleza michezo nchini linashirikisha pia wadau hivyo ni wajibu wa wanachi wote kuona michezo kuwa ni muhimu katika jamii hivyo kuwekeza katika Nyanja mbalimbali.
Hata hivyo Mhe. Shonza amewaomba wadau wote wa Michezo nchini kusaidia kushawishi makampuni,Taasisi na wadau wote kudhamini na kufadhili maendeleo ya michezo nchini ikwemo wanayoshiriki wanawake.
No comments:
Post a Comment