ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 14, 2019

Dreamliner mpya ya ATCL yafanyiwa majaribio Marekani

Ndege mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)
Ndege mpya ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) aina ya Boeing 787-8 Dreamliner iliyopewa jina Rubondo Island imeanza kufanyiwa majaribio ya kuruka. Ndege hiyo inatengenezwa na Kampuni ya Boeing nchini Marekani. Picha na Mtandao

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz


Dar es Salaam. Katika kuthibitisha kuwa Tanzania itapokea ndege mpya muda wowote kuanzia sasa, kampuni ya Boeing imeanza kuifanyia majaribio ya kuruka ndege mpya aina ya Dreamliner iliyoagizwa na Serikali.

Jana, ofisa wa kitengo cha habari cha kampuni ya Boeing, Jennifer Schuld alituma picha za ndege hiyo aina ya Boeing 787-8 na kueleza kuwa ipo kwenye majaribio.

“Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania imeanza majaribio ya kuruka leo. Ndege hii 787 inaitwa Rubondo Island,” aliandika ofisa huyo kwenye ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya Twitter ikiwa sambamba na picha kadhaa za ndege hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alipoulizwa na Mwananchi, lini ndege hiyo mpya itawasili nchini alisema bado hana taarifa rasmi ila wakati ukijiri atasema.

“Bado hatujapokea delivery note (hati ya wasilisho). Tukiipata ndio tutasema itawasili lini nchini ili wananchi wafahamu,” alisema Matindi.

Mwishoni mwa mwaka huu, ATCL inatarajia kupokea ndege mbili ikiwamo Bombardier D8-Q400 na hiyo Boeing 787-8 Dreamliner.

Mpango huo ulibainishwa na naibu waziri wa uchukuzi na mawasiliano bungeni, Atashasta Nditiye alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Khadija Nassir Ali aliyetaka kujua kama Serikali inao mkakati kuhakikisha ndege hizo zinakwenda kila mkoa wenye kiwanja na nchi jirani kusaidia kushusha gharama za usafiri wa anga.

Nditiye alisema kuwasili kwa ndege hizo kutaiwezesha ATCL kuwa na ndege za kutosha na kutoa huduma za usafiri wa anga kwa ufanisi na tija.

Ikikamilisha majaribio hayo huko Marekani inakotengenezwa, ndege hiyo mpya itawasili nchini wakati wowote.

No comments: