Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Mohamed Dewji 'MO' amempa nafasi ya kuwa mshauri wake binafsi aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Crescentius Magori.
MO katika taarifa yake aliyotoa katika mitandao ya kijamii aliandika Magori sasa atakuwa mshauri wangu binafsi katika majukumu ya kuiongoza bodi ya Simba.
MO alisema kigogo huyo aliyedumu kwa miezi nane badala ya sita katika nafasi yake ya utendaji mkuu ana uzoefu wa kutosha katika soka la Afrika sababu iliyomfanya kumpa nafasi hiyo.
Aidha MO katika mkataba ambao ameingia na Magori unaonyesha kuwa kigogo huyo anaweza kuingia katika vikao vya bodi ya klabu hiyo pale atakapohitajika.
Nafasi hiyo ya Magori haitakuwa ni ajira ya klabu hiyo bali ni makubaliano yao binafsi huku akilipwa stahiki zake zote na mwenyekiti wa bodi hiyo.
Mo Dewji alisema anaamini Magori aliiongoza Simba kufika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita atamsaidia vyema katika majukumu yake wakati anaiongoza bodi ya klabu hiyo kongwe.
Tangu aondoke Simba akiwapa taji la Ligi Kuu Bara amekuwa akihusishwa na nafasi mbalimbali akitajwa kutaka kuchukua chao cha Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania huku mwenyewe akikanusha kabla ya MO kumpa nafasi mpya.
No comments:
Post a Comment