Dar es Salaam. Akiwa na shahada tatu za uzamivu (PhD) na tatu nyingine za uzamili (masters), huenda Profesa Handley Mwafwenga ni miongoni mwa wasomi wenye shahada nyingi zaidi nchini hata duniani.
Tangu alipojiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kuhitimu diploma ya juu ya kodi (advanced diploma) mwaka 1987, Profesa Mwafwenga hajawahi kuacha kusoma kiasi cha watu wake wa karibu kumshauri apumzike kidogo.
“Askofu (Alex) Malasusa na Waziri (Palamagamba) Kabudi walinishauri nipunguze kusoma. Napenda kusoma kama wengine wapendavyo kusali, michezo au muziki,” anasema Profesa Mwafwenga ambaye hadi sasa ana digrii (shahada) saba tofauti za chuo kikuu na vyeti vingi vya kozi fupi alizosoma na kumpa mamlaka kitaaluma kuwa mchumi, mwanasaikolojia, mwanasheria na mshauri wa kodi.
Safari ya elimu ya Mwafwenga (52) ilianzia Shule ya Msingi Mwananyamala kabla hajajiunga Shule ya Sekondari Sangu na kumaliza kidato cha nne mwaka 1975.
Tangu akiwa mdogo, anasema baba yake alikuwa anamwita profesa na wakati wote alimsisitiza kusoma kwa bidii.
“Mimi ni mtoto wa mwisho. Baba yangu alikuwa mwalimu shule ya msingi. Ndiye aliyetujengea ari ya kupenda kusoma. Ndani ya nyumba yetu kuna maprofesa zaidi yangu na madokta wengi,” anasema.
Mitandaoni, India ilitikisa mwaka 2017 ilipokuwa na habari kuhusu Profesa VN Parthiban mwenye digrii tofauti 145. Huenda akawa ndiye mtu mwenye digrii nyingi zaidi duniani. Prosefa huyu alitumia miaka 30 kupata shahada hizo.
Kabla yake, mwaka 2012, Michael Nicholson alikuwa Mmarekani mwenye elimu ya juu zaidi akiwa na digrii 30 alizozipata ndani ya miaka 55 ya kusoma. Akiwa na miaka 75 wakati huo, alikuwa anatamani kufikisha digrii 33 au 34.
Ukiachana na Mmarekani huyo kutoka Jimbo la Michigan, mwaka 2010 China kulikuwa na Profesa Zhou Baokuan (74) kutoka Jimbo la Shenyang aliyekuwa na shahada tisa tofauti zikiwamo PhD tatu na shahada mbili za uzamili alizozipata ndani ya miaka 35. Katika kipindi hicho, alikuwa anafanya PhD yake nyingine Chuo Kikuu cha Fudan.
Lakini nchini Tanzania, akitumia miaka 32, Profesa Mwafwenga ameshatunukiwa digrii nyingi tofauti. Anasema muda wake wa kupumzika anautumia kusoma. Wakati wengine wanafanya mengine, yeye anasoma kitabu au chochote kitakachomuongezea maarifa.
Anasema kusoma ndio kitu anachokipenda zaidi kama ilivyo kwa wanaopenda kunywa pombe, kushabikia mpira au kuwa na wapenzi wao. Ni mapenzi haya yanayompa ujasiri wa kuendelea kusoma kila kukicha na hafikirii kuacha.
“Kwa sasa nina digrii saba. Natamani niwe nazo 10. Mara nyingi, huwa nasoma kila ninapokutana na changamoto. Sipendi kuacha kinachonishinda bila kukitafutia suluhu ya kudumu,” anasema.
Jukumu kubwa la wasomi wa ngazi za juu ni kuandika machapisho na vitabu. Yeye anasema tayari ameandika vitabu vitatu na kutoa machapisho zaidi ya 43.
Shahada alizonazo
Alipomaliza kidato cha nne, alisoma cheti cha uhasibu (National Certificate of Bookkeeping) na akaajiriwa kwa sifa hiyo.
Baada ya kufanya kazi kwa muda alijiunga na chuo cha IFM alikosoma stashahada ya juu (advanced diploma) ya kodi akigharamiwa na Wizara ya Fedha kisha akachukua diploma ya uzamili (PGD) ya kodi, akilipiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Baada ya hapo alifanya shahada ya uzamili katika usimamizi wa fedha akilipiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani halafu akamaliza na shahada ya uzamivu (PhD) katika fedha kwa gharama za Wizara ya Fedha.
“Baada ya kuona nafanya kazi nyingi zinazohusu sheria…fedha ni sheria na kodi ni sheria pia, nilirudi shule kusoma sheria,” anasema.
Sheria alisoma kuanzia digrii ya kwanza hadi PhD. Zote akijilipia mwenyewe. Kwenye sheria, anayo digrii ya kwanza, digrii mbili za uzamili na mbili za uzamivu.
Kwenye orodha hiyo pia ana shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara (MBA). Ingawa kwa wengi si kazi rahisi kupata shahada zote hizo, Profesa Mwafwenga anasema wakati mwingine alilazimika kusoma digrii mbili kwa pamoja.
“Wakati nasoma MBA ndio kipindi nilichosoma (shahada ya uzamili ya sheria) LLM. Digrii zote nimezipata hapa nchini. Sijaenda nje ya nchi hata mara moja,” anasema.
Familia na siasa
Msomi huyu ni baba wa watoto wanne, wote wa kiume na yupo karibu sana na watoto wake waliorithi tabia ya kupenda kusoma.
Anasema kutokana na kufanana tabia, wanapata muda wa kutosha kusoma pamoja na watoto wake.
“Watanzania wengi wanasoma ili kupata cheti, mpaka waone changamoto ndio wataenda kusoma ‘masters’ kama anayo digrii ya kwanza baada ya hapo, akishapandishwa cheo, haendelei tena. Mimi nasoma ili nipate maarifa,” anasema.
Wakati mwingine, anasema huwa anachukua wasifu wake na kuutathmini na akiona kuna upungufu wowote basi anaenda kusoma.
Hata akiwa kazini na kukawa na kitu kinamsumbua, hurudi shule kunoa uwezo wake.
“Nilipohitimu masomo ya kodi muda mwingi nilikuwa nakutana na wanasheria, niliona kuna vitu haviko sawa hivyo nikarudi shule kusoma sheria ili nizungumze nao lugha moja,” anasema.
“Nilipokuwa Wizara ya Nishati na Madini nikaona nisome ‘masters ya accounting in oil and gas’ kwa kuwa ndivyo vitu vilikuwa vinaleta changamoto wakati huo.”
Profesa Mwafwenga anayevutiwa na siasa pia anasema ameshagombea ubunge wa Afrika Mashariki mara mbili kupitia CCM bila mafanikio.
Hasomi tu, hufanya mambo mengine pia kila apatapo wakati. Kwa nyakati tofauti anasema ameshakuwa mshereheshaji na mchangiaji kwenye magazeti mbalimbali.
“Nimekuwa MC, nimepiga muziki nikiwa na Zahiri Ally Zorro na wengineo. Nimekuwa mwandishi wa habari pia nikiandikia gazeti la Majira. Kati ya mwaka 1997 na 2001 nikahamia Mwananchi. Nimeandikia Uhuru pia,” anasema.
No comments:
Post a Comment