ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 24, 2019

Rugemalira mgonjwa, ashindwa kufika mahakamani

By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. James Rugemalira, mshtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kwa maelezo kuwa ni mgonjwa.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon ameieleza mahakama hiyo leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Rugemalira ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL pamoja na mwenyekiti mtendaji wa PAP, Habinder Seth wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya kutakatisha fedha.

Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shaidi kuwa amepata taarifa Rugemalira ni mgonjwa na leo ameshindwa kuletwa mahakama kwa ajili ya kusikiliza kesi yake.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa upelelezi bado haujakamilika tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Simon.

Kuhusu maombi ya washtakiwa kukiri makosa na kuomba msamaha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), wakili Simon amesema maombi hayo bado yanaendelea kufanyiwa kazi.

Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 7, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Wawili hao wanaendelea kusota rumande kwa muda wa miaka miwili sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu , kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309 bilioni

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam ambako wanadaiwa kula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

No comments: