ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 25, 2019

Rwanda yakomalia kituo cha nyuklia, wapinzani wapinga

Kigali. Uamuzi wa Rwanda kutiliana n saini na kampuni ya Urusi kuhusu ujenzi wa kituo cha nyuklia nchini humo umeanza kupata upinzani kutoka chama cha upinzani.

Urusi imeahidi kusaidia baadhi ya mataifa ya Afrika kujenga uwezo wake wa kutumia teknolojia ya nyukilia ilipokutana na mataifa 40 ya Afrika katika mkutano uliomalizika katika mji wa Sochi nchini humo.

Miongoni mwa mataifa yanayotarajiwa kunufaika kwa ushirikiano huu, ni Rwanda ambayo tayari imesaini makubaliano Kampuni ya atomiki ya Rosatom ya Urusi kujenga kituo cha sayansi na teknolojia ya nyuklia katika harakati za kampuni hiyo kutanua shughuli zake Afrika.

Kutokana na uamuzi huo, Frank Habineza, kiongozi wa chama cha upinzani cha Green nchini Rwanda amepinga mpango wa nchi hiyo kujenga kiwanda cha nyuklia akisema utakuwa na athari mbaya kwa wananchi.

Habineza amenukuliwa na BBC akisema wapinzani nchini humo hawakuunga mkono ushirikiano huo baina ya serikali ya Rwanda na Urusi kutokana na athari zake.

"Kulikuwa na mapatano ya Vienna kuhusu masuala ya nyuklia, na wakati huohuo Rwanda ilisaini mapatano mengine na Urusi kuanzisha kiwanda cha nyuklia hapa Rwanda. Mapatano ya Vienna yalikuwa kama kupalilia njia ya hayo ya Urusi kuanza kutekelezwa, amesema Habineza, mbunge katika Bunge la Taifa kupitia chenye uwakilishi wa viti viwili bungeni.

Alisema wao hawakupigia kura muswada huo kwa sababu waliona ni mapema kwa Rwanda kujiingiza katika kuidhinisha matumizi ya nishati ya nyuklia kwa sababu sehemu zote ilikojengwa nyuklia kumekuwa na athari mbaya kwa wananchi na kwa mataifa yenyewe.

Kiongozi huyo wa upinzani ametaja mfano wa Ukraine ambako kiwanda cha nyuklia kililipuka na kuathiri nchi jirani ya Sweden.

Muswada huo wa ujenzi wa nguvu za nyuklia ulipitishwa bungeni Rwanda ukipingwa na wabunge wawili pekee.

Lakini Serikali ya Rwanda inasema teknolojia ya nyuklia itaifaa kwa matumizi ya kutengeneza nishati, dawa na matumizi mengine ya amani.

Shughuli za kituo


Kituo hicho kitafanya tafiti za kisayansi na “majaribio” ya teknolojia ya nyuklia na kusalisha kemikali maalumu zitakazosaidia katika shughuli za kilimo ambazo husaidia kuzalisha mazao yanaohimili ukame na magonjwa, yenye viwango vya juu na yanayotoa mazao mengi kwa muda mfupi.

Kwa mkataba huo, Rosatom ambayo ni kampuni kubwa ya nyuklia yenye mikataba ya nje ya nchi kuliko kampuni zote, ina matumaini itaweza kuisaidia Rwanda kupata nishati ya umeme wa nyuklia.

Kampuni hiyo ina vituo 36 katika nchi za Bangladesh, Belarus, China, Misri, Finland, Hungary, India na Uturuki.

Pia kwa mujibu wa Reuters, Rosatom imesema imekubaliana na Ethiopia kushirikiana katika kuendelea miundombinu ya nyuklia.

Vilevile, kampuni imekuwa katika mazungumzo na Afrika Kusini kuhusu ujenzi wa vinu zaidi vya nyuklia nchini humo lakini Rais Cyril Ramaphosa amesitisha kwa muda uendelezaji wa shughuli za nyuklia.
MWANANCHI

No comments: