ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 7, 2019

Ukibaini ‘mchawi’ wa maisha yako ni wewe, fanya hivi!


NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana tena kupitia safu hii ambayo naamini imewasaidia wengi kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha.

Ushauri wangu kwako ni kuhakikisha kila ninachokiandika unakifanyia kazi. Utakuwa ni mtu wa ajabu sana kama utakuwa ni mdau wangu halafu maisha yanakuchanganya. Hata kama linalokusumbua sijaligusia katika makala zangu, nipigie kwa namba zilizopo hapo juu tushauriane.

Baada ya kugusia kidogo hayo, sasa nirudi kwenye mada yangu niliyokuandalia kwa wiki hii. Iko hivi, baadhi ya watu huamini uchawi. Wengine huenda mbali zaidi na kuamini katika kujikinga na uchawi. Wachache kati yao huamua kabisa kuwa wachawi!

Hayo ni makundi matatu katika jambo moja, uchawi. Kwa tafsiri nyepesi, uchawi ni nguvu ya kuzuia jambo au kudhuru mwingine. Yaani ni uwezo wa kumfanya mwingine akwame kufikia lengo fulani.

Inaweza kuwa afya, mafanikio nk. Katika maisha wakati fulani unaweza kukwama kufikia malengo yako kwa sababu mbalimbali, lakini wengine huanza kufikiri huenda kuna ‘wachawi’ wa maisha yao ndiyo maana hawafanikiwi.

Katika mafanikio na ujasiriamali, tunaamini hicho ni kiwango cha juu cha ujinga. Mtu mwenye akili timamu, hata siku moja hawezi kukesha akisaka mchawi wa maisha yake. Zaidi, ukijichunguza sana, utakuja kugundua mchawi wa maisha yako ni wewe mwenyewe.

Wapo wengi ambao waliishi maisha ya ufukara kwa muda mrefu, hadi pale walipoamua kubadili namna ya kuwaza; kuamini kwamba, wachawi wa maisha yao ni wao wenyewe, ndipo walipofungua njia za mafanikio yao.

Unaweza kumsikia mtu mzima na akili zake anasema; “Mimi nisingekuwa hivi kama siyo wazazi wangu. Wamenizaa, hawajanisomesha ndiyo maana sipati kazi mahali popote. Kama ningezaliwa familia tajiri nisingekuwa hivi.”

Mwingine anasema; “Nimezaliwa kwenye familia duni, wazazi wangu wanakaa nyumba ya kupanga na wamekufa wametuachia umaskini, kama siyo wao, ningekuwa mbali.”

Ndugu yangu, fungua ubongo wako leo, hakuna mchawi wa maisha yako. Ukitaka kufanikiwa, unatakiwa kuacha kulalamika na kuanza kutenda.

Kama unadhani elimu ndiyo njia pekee ya mafanikio, nenda Kariakoo kachunguze wafanyabiashara wakubwa wenye maduka ya mabilioni kama waliona hata kidato cha kwanza! Ndugu zangu, sisemi kwamba elimu haina maana katika maisha yetu ya sasa, lakini isiwe kikwazo kwako, kwamba bila elimu usingekuwa ulivyo.

Kumbukumbu zangu zinaonesha kwamba, matajiri wengi duniani walitoka familia duni, lakini pia hawana elimu kubwa. Baadhi ya matajiri ambao waliamua kuweka historia zao hadharani, wanakiri kwamba walikuwa ‘bongolala’ darasani.

Jambo kubwa na la msingi kwako ni kuanza kufukuzia ndoto zako. Amini uwezo wa akili yako. Mradi upo hai, mengine yanawezekana ndugu zangu. Mshukuru Mungu kwa pumzi ya uhai aliyokupa bure kisha inuka na uanze kupambana.

Kama umeshakubali kuwa mchawi wa maisha yako ni wewe mwenyewe, ni jambo zuri. Sasa ni kazi yako kujiagua mwenyewe. Angalia fikra zako zina nini? Kama ni kweli unadhani elimu ndiyo kikwazo kwako, anza kusoma.

Zama hizi za sayansi na teknolojia, kila kitu kimerahisishwa. Ikiwa wazazi wako hawajakusomesha na unaamini katika shule, hujachelewa. Zipo programu nyingi za kusoma kuanzia elimu ya awali ya sekondari, elimu ya juu ya sekondari, vyuo vikuu nk. Ni wewe tu, ratiba yako na ada yako.

Lakini ndugu zangu, niwaeleze ukweli, katika maisha yetu wapo baadhi ya watu ni ‘wachawi’. Hawa ni wale wanaotukatisha tamaa, wanaotusengenya na kutusema vibaya nk. Jitahidi kadiri unavyoweza kukaa mbali na watu wa namna hii.

Hawa watakurudisha nyuma. Kuna vitu vingi vya kufanya katika maisha, ukitenga muda wa kuwasikiliza watu wa namna hii watakuvuta shati. Maisha ni wewe mwenyewe, usikubali mwingine ayaharibu maisha yako.

Mtaalam mmoja wa kutia hamasa za mafanikio nchini Tanzania, James Mwang’amba, alipata kusema; “Ukiwa na mtu mmoja anayekuambia huwezi, ili uweze kuondoa hiyo sumu ya ‘huwezi’ akilini mwako, lazima wapatikane watu wengine ishirini watakaokuambia unaweza.”

Hapo unaweza kuona ni hatari kiasi gani, kuwa na urafiki na watu wa namna hiyo. Mwang’amba anasema, hata kama ni ndugu yako, achana naye, ingawa ameonesha ugumu wa kuachana na ndugu, lakini akamalizia kusema; “…basi punguza time ya kuwa nao.”

Nadhani umenielewa, ni wakati wa kufanyia kazi hiki nilichokiandika kisha tukutane tena Ijumaa.

No comments: