Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mfanyabiashara Hamis Said (38) anayedaiwa kumuua Naomi Marijani na kumchoma moto wa mkaa, umedai kuwa jalada lipo kwenye hatua ya uchapaji.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi umekamilika.
Simon amedai kuwa jalada lipo kwenye hatua ya uchapishaji hivyo anaiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.
"Kama nilivyoongea tarehe iliyopita jalada lipo kwenye hatua ya uchapishaji hivyo shauri hilo litakapokuja tena nitaijulisha mahakama imefikia wapi," amedai Simon.
Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally aliahirisha shauri hilo hadi Novemba 18, 2019 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Anayedaiwa kumuua mkewe kisha kumchoma moto awatolea uvivu waandishi wa habari mahakamani
Mshtakiwa huyo ameshtakiwa chini ya Kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Katika kosa hilo, mshitakiwa anadaiwa Mei 15, 2019 katika eneo la Gezaulole Kigamboni Dar es Salaam alimuua mtu anayeitwa Naomi Marijani.
Inakumbukwa kuwa Hamis anadaiwa kumuua mke wake Naomi kisha kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa ambapo alichukua majivu ya marehemu na kwenda kuyafukia shambani kwake.
No comments:
Post a Comment