Dar es salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliyemaliza muda wake, Profesa Mussa Assad amesema hafahamu na hakuwahi kufikiri kama angeweza kutengeneza adui wakati wa utekelezaji wa majukumu yake akiwa katika ofisi hiyo.
Profesa Assad amesema huenda waliotengeneza uadui kwake ni kundi la watumishi waliokuwa wanakwenda kinyume na misingi yake ya kazi.
“I have never intentionally made an enemy, Sijawahi hata siku moja kufikiria ninatengeza uadui, inawezekana kuna watu niliwakwaza lakini ni kwa sababu ya kutosimamia misingi ya kazi,” amesema Profesa Assad.
Ametoa kauli hiyo leo Novemba 4, 2019 alipoulizwa na Mwananchi kama amesamehe wote aliokwazana nao wakati wa majukumu yake akiwa CAG.
Alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa walioshiriki Kongamano la sita la Taasisi za Kifedha za Kiislamu barani Afrika lililofanyika leo Jumatatu, Novemba 4, 2019 Jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, hakutaka kuzungumzia chochote kuhusu changamoto za ofisi hiyo, uteuzi wa anayerithi mikoba yake, wala kugusia tofauti zake na muhimili wa Bunge.
Amesema kutokana na misimamo yake ya kujali misingi ya kazi, amewahi kuwafukuza kazi watumishi wanne akiwamo rafiki yake baada ya kuthibitisha tuhuma za wizi.
“Sasa hao ndiyo wanaweza kunichukulia kama adui yao lakini kwa sababu ya misingi ya kazi, nafikiri kusameheana ni muhimu sana kwa watu wote,” amesema Profesa Assad.
No comments:
Post a Comment