Tume hiyo ilibuniwa ili kuchunguza madai ya unyanyasaji dhidi ya Jammeh wakati wa kipindi chake cha utawala wa miaka 22.
Ripoti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza imesema ushahidi wa Fatou Jallow, ulikamilisha kikao cha wiki tatu kilichosikiliza tuhuma za udhalilishaji wa kingono.
Jammeh alitoroka Gambia 2017 baada ya kukataa kustaafu baada ya kushindwa kwake katika uchaguzi wa urais.
Kwa sasa anaishi mafichoni nchini Guinea ya Ikweta.
Ushahidi wa Fatou Jallow ni miongoni mwa ripoti ya shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch ambayo inaelezea madai mengine dhidi ya Jammeh ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono.
BBC ilijaribu kuwasiliana na Jemmeh binafsi huko Equitorila Guinea bila mafanikio lakini msemaji wa chama chake cha APPR, kwa niaba yake alikana madai hayo yaliyotolewa dhidi ya Jammeh.
“Sisi kama chama na raia wa Gambia tumechoka na msururu wa madai ambayo yameripotiwa dhidi ya rais wa zamani,” alisema Ousman Rambo Jatta katika taarifa iliyotumwa kwa BBC.
"Rais huyo wa zamani hana muda wa kujibu uongo na kampeni za kumuharibia jina. Ni mtu anayemuogopa Mungu ambaye anaheshimu sana wanawake wa Gambia,” alisema naibu wa kiongozi wa chama hicho cha APPR.
Mapema, Jallow alisema alitaka kukutana na Jammeh mwenye umri wa miaka 54 mahakamani ili ashtakiwe.
''Nimejaribu sana kuficha na kufutilia mbali habari hiyo na kuhakikisha kuwa haitakuwa moyoni mwangu. Kwa kweli sikuweza, hivyo basi nikaamua kuzungumza,” alisema.
Ushahidi wake
Jallow alisema kuwa alikuwa na umri wa miaka 18 wakati alipokutana na Jammeh baada ya kushinda shindano la malkia wa urembo mwaka 2014 katika mji mkuu wa Banjul.
Miezi kadhaa baada ya kupata taji hilo, anasema rais huyo wa zamani alijifanya kama mzazi wakati alipokutana naye akimpatia ushauri, zawadi na fedha na kuandaa maji kupelekwa katika nyumba yao ya familia.
Na katika chakula cha jioni kilichoandaliwa na msaidizi wa rais huyo, anasema alimuuliza iwapo wangeoana.
Yeye alikataa wazo hilo mbali na zawadi alizokuwa akipatiwa.
Jallow anasema kuwa msaidizi huyo baadaye alisisitiza kwamba anafaa kuhudhuria sherehe ya kidini katika ikulu ya rais kama malkia wa urembo Juni 2015.
Lakini alipowasili alipelekwa katika makazi binafsi ya rais huyo.
“Ilikuwa wazi kile ambacho kingetokea,” alisema mrembo huyo akitaja hasira za Jammeh baada ya yeye kukataa kufunga naye ndoa.
Jallow anasema alipigwa kofi na kudungwa sindano katika mkono wake.
“Alifuta sehemu zake za siri katika uso wangu, akanisukuma nipige magoti na kunifanyia vibaya,” alilalamika.
Msichana huyo baadaye alisema alijifungia nyumbani kwao kwa siku tatu na kuamua kutorokea Senegal.
Alipokuwa Dakar, mji mkuu wa Senegal, Jallow alitafuta msaada wa mashirika kadhaa ya haki za binadamu.
Wiki chache baadaye, anadai alipatiwa ulinzi na kupelekwa Canada ambapo amekuwa akiishi tangu wakati huo.
Mfumo wa unyanyasaji
Shirika la Human Rights Watch (HRW) na Trial International yanasema Jammeh alikuwa na mfumo wa kunyanyasa wanawake na wengine walikua wakilipwa mshahara na serikali na kufanya kazi katika ikulu kwa jina la 'wasichana wa itifaki'', ambao walikuwa wakifanya kazi za ukarani lakini umuhimu wao mkubwa ulikuwa kushiriki ngono na rais.
Mwanamke mwingine ambaye aliajiriwa kama ofisa wa itifaki akiwa na umri wa miaka 23 anasema naye alilazimishwa 'kushiriki' ngono na Jammeh mwaka 2015.
Mwanamke huyo ambaye aliomba kutofichuliwa jina, alisema siku moja rais huyo alimwita chumbani mwake.
“Alianza kunivua nguo na kusema alikuwa ananipenda, angenifanyia chochote ningetaka na familia yangu, na kwamba nisimwaambie mtu yeyote na iwapo nitakiuka hilo nitakiona cha mtema kuni.
''Nilihisi sina chaguo. Siku hiyo alilala nami bila kutumia kinga yoyote''.
Mwanamke mwingine ambaye alifanya kazi kama ofisa wa itifaki alisema hata yeye alijua kwamba iwapo mmoja wao angeitwa kwa Rais ingekuwa kwa sababu ya kushiriki ngono.
“Wengine walikuwa wanataka. Walihisi kuheshimiwa au walitaka pesa, aliambia shirika la haki za kibinadamu la HRW akificha jina lake,” alisema.
Alielezea vile alivyonyanyaswa kingono na rais huyo nyumbani kwake huko Kanilai, 2013 wakati alipokuwa na umri wa miaka 22.
"Jioni moja, msaidizi mmoja wa rais aliniita na kuandamana naye katika nyumba ya binafsi ya rais. Alinitaka kuvua nguo, aliniambia kwamba mimi ni msichana mdogo niliyehitaji ulinzi na alitaka kunipaka maji ya kiroho.”
Katika kisa kingine siku iliyofuata, alianza kulia wakati Jammeh alipoanza kumshika mwili wake.
Anasema kwamba baadaye alifutwa kazi huku ahadi ya kupata ufadhili wa masomo ikifutiliwa mbali.
Rais Adama Barrow amesema atasubiri ripoti hiyo ya tume ya maridhiano kabla ya kuamua iwapo atamrudisha Jammeh nyumbani kutoka mafichoni nchini Guinea ya Ikweta. MWANANCHI
No comments:
Post a Comment