ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 17, 2019

habari picha kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais

Washiriki wa Mafunzo ya Msasa ya kuhusu Uwezeshaji Mashamba darasa kwa Maafisa viungo wa mradi kutoka Wizara na timu za uwezeshaji za wiakiwa katika mafunzo kwa vitendo.

Sehemu kubwa ya Watanzania hutegemea shughuli za kilimo kwa ajili ya chakula na biashara na hivyo ni mchango mmojawapo wa uchumi wa Taifa.

Pia Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wakulima wananufaika nma shughuli hizo za kilimo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kwa kilimo cha mazao tofauti tofauti

Hata hivyo pamoja na juhudi hizo za Serikali bado wakulima wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli zao za kilimo na hivyo kupata wakati mgumu.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na changamoto ya uharibifu wa ardhi ambayo inayoleta athari kwa kilimo hali inayochangia uzalishaji duni wa chakula.

Hali hiyo hutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanyika zikiwemo zikiwemo kuharibu vyanzo vya maji na ukataji miti kwa ajili ya kuni au uchomaji wa mkaa hali inayochangia uharibifu wa mazingira.

Kutokana na changamoto hizo, Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ina dhamana ya usimamizi wa mazingira inaratibu na kutekeleza Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS) hapa nchini.

Mojawapo ya malengo ya mradi huo ni kuboresha mifumo ya ikolojia ya kilimo ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji wa chakula na kuchangia kuboresha mazingira katika wilaya husika.

Miongoni mwa wilaya ambazo mradi huo unatekelewa ni nne za Tanzania Bara ambazo mikoa yake iko kwenye mabano ni pamoja na Kondoa (Dodoma), Mkalama (Singida), Nzega (Tabora) na Magu (Mwanza). Pia unatekelezwa katika wilaya moja kwa upande wa Tanzania Zanzibar ambayo ni Micheweni (Pemba).

Hivi karibuni Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa mafunzo msasa ya uwezeshaji kuhusu mashamba darasa kwa maafisa viungo wa mradi kutoka Wizara na timu za uwezeshaji za wilaya wa mradi huo.

Mfunzo hayo yatakuwa msaada mkubwa kwa maafisa hao ambao wataitumia elimu waliyoipata katika kufanikisha uanzishaji wa mashamba darasa katika maeneo ya mradi.

Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamekuwa wakitekeleza miradi inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo kwa kusogeza karibu teknolojia kwa wakulima, lengo likiwa ni kuongeza usalama wa chakula na kuongeza kipato cha jamii.

Hizi ni juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inahusisha uingizaji na matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea, mbegu zenye ubora, uboreshaji wa nyanda za malisho na utoaji wa huduma za ugani na mafunzo kupitia shamba darasa.

Hivyo kutokana na mukhtadha huu juhudi hizi zote zina lengo la urejesha ardhi iliyoharibika ili iweze kuendelea kuzalisha mazao ya kilimo, mifugo na misitu hapa nchini.

Mratibu wa mradi kutoka Ofisi hiyo, Joseph Kihaule anasema kuwa mradi huo unajumuisha uanzishwaji wa mashamba darasa 100 katika wilaya hizo Tanzania Bara na Zanzibar.

Wawezeshaji wa mradi huo ni Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Wakala wa Taifa wa Mbegu za Miti Tanzania (TTSA) huku washiriki wa mafunzo wakitoka taasisi mbalimbali za Serikali.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Wizara za Kilimo, Maliasili na Utalii, Maji, Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Idara ya Mazingira, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar.

Wengine ni kutoka katika Halmashauri zinazotekeleza mradi huo huku mikoa ikiwa kwenye mabano ni Mkalama (Singida), Micheweni (Pemba), Magu (Mwanza), Nzega (Tabora) na Kondoa (Dodoma).

Mradi huu umenufaisha Watanzania kwa kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi iliyoandaliwa ambayo itawasaidia kuwa na usimamizi bora wa maliasili, matumzi endelevu ya ardhi na kupungua kwa migogoro ya matumzi ya ardhi na maliasili.

Aidha, mradi huu umewezesha wananchi kupatiwa mikopo kwenye taasisi za fedha, kuandaa mafunzo kuhusu upangaji wa matumizi ya ardhi yamewajengea uwezo wa upangaji na usimamizi wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao.

Pamoja na hayo pia mradi umesaidia katika uboreshaji wa hali za maisha ya wananchi kwa matumizi ya taarifa za awali za utafiti lakini pia wataalamu wamejengewa uwezo wa uanzishaji na uendeshaji wa mashamba darasa.

Kazi zilizofanyika hadi sasa katika utekelezaji wa mradi

Miongoni mwa kazi zilizofanyika ni kuundwa kwa Kamati za usimamizi wa Maliasili na Mazingira, Kamati za Mipango Bora ya Matumizi ya Ardhi za vijjiji katika vijiji vyote vya mradi isipokuwa wilaya ya Micheweni ambako Kamati za Mipango Bora ya Matumizi ya Ardhi za shehia hazijaundwa.

Pia yameendeshwa mafunzo ya upangaji wa matumizi ya ardhi kwa maafisa wa ngazi ya wilaya na vijiji, wajumbe wa Kamati za Mipango ya Matumizi ya Ardhi za vijjiji, Halmashauri za Vijiji na baadhi ya wananchi na jumla ya maafisa na wanavijiji 821 wamepata mafunzo hayo.

Kufanya Tathmini ya utambuzi wa vyanzo vya maji na teknolojia zitakazotumika kupata maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu, kilimo na mifugo katika vijiji vyote vya mradi katika wilaya za Mkalama, Nzega, Magu na Kondoa.

Kuandaa Mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 15 kwenye wilaya za Mkalama (vijiji vitano), Nzega (Vijiji vitano), Kondoa (vijiji viwili) na Magu (vijiji vitatu). Uainishaji wa Vipaumbele vya maeneo na makundi ya watumiaji raslimali kwa ajili ya urejeshwaji wa uoto wa asili na hifadhi ya bioanuai umefanyika na kukubalika na wadau katika vijiji vyote vilivyoandaa mipango ya matumizi ya ardhi.
Muda wa kutekeleza mradi huu ni kwa kipindi cha miaka mitano (2017-2022) na gharama ya mradi ni Dola za Marekani millioni 7.156. Mfadhili mkuu ni Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).

No comments: