Dar es Salaam. Mshambuliaji mpya wa Yanga, Ditram Nchimbi amefunguka sakata lake lililopelekea kuwekewa pingamizi na klabu ya Polisi Tanzania aliyokuwa akicheza kwa mkopo akitokea Azam.
Nchimbi ambaye leseni yake kuichezea Yanga ilizuiwa tayari amepata leseni hiyo saa chache zilizopita na atakuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba.
Juzi kaimu katibu mkuu wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema wameweka pingamizi TFF, mshambuliaji huyo kusajiliwa na Yanga msimu huu wa dirisha dogo kwa kuwa walimpa fedha anazotakiwa kuzirejesha ili zitumike kusajili mchezaji mwingine.
Akizungumzia suala ilo Nchimbi alisema alikiri kuwa na makubaliano na Polisi Tanzania, lakini amesema kabla ya kutua Yanga waliyamaliza.
"Niliongea nao kabla tukamalizana, lakini mambo ya mpira yana vitu vingi ndiyo sababu nyuma yakaibuka yaliyoibuka, ila kikubwa nashukuru sakata hilo limekwisha na nimepata leseni kuanza kuitumikia Yanga," alisema.
Alisema kila kitu kina tokea kwa sababu, hivyo anaamini hata suala lake kucheza Yanga limekuja kwa sababu.
"Uenda ilipangwa mechi ya Simba na Yanga iwe mechi yangu ya kwanza kucheza nikiwa na Yanga ndiyo sababu yote yaliyotokea yametokea," Nchimbi ameiambia MCL Digital Leo.
Sakata la Nchimbi
Maafande wa Polisi Tanzania walimemwekea pingamizi Nchimbi na kusababisha kukosa kibali cha kuanza kuitumikia Yanga iliyomsajili kutoka kwa Azam waliokuwa wakimliki kwa mkataba wa miaka miwili uliokuwa umesaliwa miezi michache kabla ya kumalizika kwake.
Ipo hivi. Yanga iliomba leseni kutoka Shirikisho la Soka (TFF) ili Nchimbi na wenzake waliosajiliwa kwenye dirisha dogo akiwamo Adeyun Saleh na Tariq Seif ambao jana walianza mambo yao wakati Yanga ikivaana na Biashara United, lakini ishu la Nchimbi likapata kikwazo na leseni kutotolewa.
Leseni za Adeyun na Tariq ndizo pekee zilizotolewa huku leseni ya Nchimbi ikizuiliwa kwa madai kuwa, Polisi wameamua kukomaa nao wakitaka walipwe fedha walizomkopesha wakati akiichezea timu yao kwa mkopo kutoka Azam.
Inadaiwa Polisi walimkopesha nyota huyo aliyewahi kutamba na timu za Njombe Mji, Mwadui na Majimaji kiasi fulani cha fedha (kiwango kimehifadhiwa kwa sasa) na wanataka walipwe kwanza.
Uongozi wa Yanga kupitia Msemaji wake, Hassan Bumbuli aliyekuwa akifuatilia suala la wachezaji wao wapya, alisema waliambiwa na TFF kuna madai kutoka Polisi kuhusiana na mchezaji huyo na wanatakiwa kukaa meza moja ili kufikia muafaka.
“Ili suala limetushangaza sana... hivi mchezaji alikuwa mali ya nani, Azam au Polisi? Mpaka sasa hatujui mantiki ya TFF kuzuia leseni yake kwani tulifuata taratibu zote za kumpata kutoka Azam FC,” alisema Bumbuli.
Kauli ya TFF
Afisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema hana taarifa kuhusiana na sakala hilo na kusukuma mzigo kwa mkurugenzi wa mashindano, Salum Madadi ambaye pia alisema hana taarifa hizo.
“Sina maelezo ya kina kuhusiana na suala hilo, naomba uwasiliane na Kidifu (Herman) ambaye ataelezea suala hilo kisheria,” alisema Madadi.
Hata hivyo, Kidifu alikataa kuzungumzia suala hilo na kusema yeye si msemaji wa TFF.
“Naomba wasiliana na Madadi na umwambie anipigie ili nimuelezee sakata hilo na yeye azungumze, mimi si msemaji wa TFF,” alisema Kidifu.
Baada ya kurejea tena kwa Madadi, naye alisema kuwa si msemaji wa suala hilo, jambo ambalo linadaiwa pengine inatokana na kukwepa presha na lawama kuelekea pambano hilo la watani.
WASIKIE POLISI
Kaimu Katibu Mkuu wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alithibitisha kuweka pingamizi TFF kupinga mchezaji huyo kuichezea Yanga kutokana na kuingia makubaliano na mchezaji na klabu ya Azam.
Lukwaro alisema kuwa walimuomba Nchimbi kutoka Azam kwa barua na klabu hiyo kuwajibu kwa barua, jambo ambalo liliwapa nafasi wao kumtumia mwaka mzima.
Alisema kuwa kuna kiasi cha fedha walimpa mchezaji kwa kukubali kuichezea timu yao na madai yao makubwa ni kuwataka Yanga kuja mezani na kupata muafaka wa sakata hilo.
“Nchimbi mwenyewe anajua kiasi cha fedha tulizompa kutokana na makubaliano maalum, hizi ni fedha za serikali, haziwezi kupotea hivi hivi, lazima suala hili lijadiliwe kwa pande zote mbili,” alisema Lukwaro.
Alisema kuwa Azam pia wanajua makubaliano yao pamoja na kumiliki mchezaji kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu.
“Nikija kwako kuazima gari na kuingia makubaliano, unawezaje kuja kuchukua gari hilo bila ya muda tuliokubaliana kumalizika hata kama ni mali yako, lazima ufuate utaratibu tuliowekeana, sisi hatuna nia ya kumtumia Nchimbi,” alisema Lukwazo.
No comments:
Post a Comment