ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 30, 2019

TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA SH. BILIONI 4.2 KUTOKA JAPAN KWA AJIRI YA KUFUFUA SHIRIKA LA TAFICO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia), na Naibu na Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Katsutoshi Takeda, wakisaini mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia), na Naibu na Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Katsutoshi Takeda, wakibadilishana mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ambapo TAFICO itaweza itaweza kuwa na Meli ya Uvuvi, hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (kulia), na Naibu na Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Katsutoshi Takeda, wakiwa wamenyenyua Mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wakuu wa Idara na Maafisa waandamizi (mbele) kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakishuhudia kusainiwa kwa mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (katikati) akieleza kuhusu misaada na mikopo yenye masharti nafuu inayotolewa na Japan, wakati wa hafla ya kusainiwa kwa Mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Katsutoshi Takeda na kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa upande wa Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa upande wa Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah, akielezea jitihada za Serikali za kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James (wa pili kulia), na Kaimu Balozi wa Japan nchini Tanzania, Bw. Katsutoshi Takeda (wa tatu kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Tanzania na Japani baada ya hafla ya kusainiwa kwa mkataba wa Msaada wa Sh. 4.2 kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), Jijini Dar es Salaam.

NA PETER HAULE, WFM

TANZANIA imepokea msaada wa Yen za Japan milioni 200 sawa na Shilingi Bilioni 4.2 kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO)

Mkataba wa msaada huo umesainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu na Kaimu Balozi wa Japan, Bw. Katsutoshi Takeda, kwa niaba ya Serikali ya Japan.

Katibu Mkuu, Bw. Doto James, alisema kuwa msaada huo utatumika kununua Meli ya Uvuvi yenye vifaa vya kisasa, mashine ya kutengeneza barafu, ghala la baridi la kuhifadhia samaki, Vifaa mbalimbali vya kuvulia samaki na vya karakana, gari lenye mitambo maalum ya barafu na Gari kwa ajili ya kusambazia samaki.

Alisema kuwa utekelezaji wa Mradi huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Pili (FYDP II), ambayo pamoja na mengine unalenga kuboresha Sekta ya Uvuvi na hatimaye kuvutia Watanzania zaidi kujihusisha katika Sekta ya Uvuvi kama shughuli kuu ya kujipatia kipato.

“Mradi huu utaongeza uuzaji wa samaki nje ya nchi, kuongeza uhakika wa chakula nchini, na pia utaboresha usindikaji wa samaki, kuongeza thamani na masoko na kupunguza upotevu wa mazao ya samaki baada ya kuvua”, alieleza Bw. James.

Alisema kuwa Kiwango cha ukuaji kwa shughuli ndogo za kiuchumi za uvuvi kilifikia asilimia 9.2 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.4 mwaka 2017 ambapo kiwango kikubwa cha ukuaji kilitokana na utunzaji mzuri wa mazalia ya samaki yakiwemo mabwawa ya watu binafsi sambamba na kuongezeka kwa mahitaji katika soko la ndani na nje.

Bw. James alisema kuwa, shughuli za uvuvi zilichangia asilimia 1.7 katika Pato la Taifa mwaka 2018, ambayo inadhihirisha umuhimu wa uvuvi katika uchumi, hivyo msaada uliotolewa utachangia jitihada za Serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Malengo Endelevu ya mwaka 2030 na Agenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063.

Alisema kuwa Serikali ya Japan imekuwa ikiisaidia Tanzania kupitia misaada na mikopo nafuu katika Sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo, Miundombinu ya barabara, Maji, Nishati Utawala Bora na Uwajibikaji ambapo mpaka sasa Jumla ya Sh. Trilioni 1. 3 zimetolewa na Serikali hiyo tangu mwaka 2012.

Misaada na mikopo hiyo inadhihirisha kuwa kuna uhusiano mzuri wa kirafiki kati ya Tanzania na Serikali ya Japan, hivyo matumaini ni kuwa urafiki huo utaendelea kuimarishwa na Serikali zote mbili kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizo.

Kwa upande wake Naibu na Kaimu Balozi wa Japan, Bw. Katsutoshi Takeda, kwa niaba ya Serikali ya Japan amesema nchi yake itaendelea kuisaidia Tanzania kutokana na ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili lakini pia kuchangia jitihada za Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi na kuondoa umasikini wa wananchi wake.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamahtamah ameishukuru Serikali ya Japan kwa msaada huo utakaosaidia kufufua Shirika hilo la Uvuvi.

Alisema kuwa Serikali itapeleka mswaada Bungeni mwezi Januari mwakani, ili kuliwezesha TAFICO kuanza kazi zake rasmi na kwa kishindo ili Shirika hilo liweze kuchangia katika uchumi wa Taifa kwa kiwango kikubwa.

Alisema kuwa pamoja na msaada huo, Serikali imechukua hatua za kuchambua mali zilizokuwa zikimilikiwa kinyemela na baadhi ya taasisi na watu ambapo mpaka sasa mali zenye thamani ya zaidi shilingi bilioni 118 zimerejeshwa Serikalini na kazi ya kurejesha mali nyingine zinaendelea kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina.

No comments: