ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 25, 2019

Wanafunzi 300 wapata ujauzito kwa mwaka huu Dodoma

By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

Dodoma. Wanafunzi 304 wa shule za msingi na sekondari wamepata mimba mkoani Dodoma na kukatiza masomo kati ya Januari na Desemba.

Hii ni sawa na wanafunzi 25 kwa mwezi walipata ujauzito na kuacha masomo yao, kati yao 237 ni wa sekondari na 67 ni wa msingi.

Akiwasilisha taarifa ya elimu kwenye kamati ya ushauri mkoa, ofisa Elimu wa mkoa wa Dodoma, Maria Lyimo alisema idadi hiyo imechukuliwa kuanzia Januari hadi Desemba.

Maria hakutaja takwimu za waliopata mimba mwaka 2018, lakini alikiri kuna tatizo kubwa eneo hilo.

Alisema mimba ni moja ya matatizo yanayokwamisha ukuaji elimu mkoani Dodoma na kuitaka Serikali na wadau wengine kusaidia mikakati ya kupunguza hali hiyo.

Alitaja tatizo lingine ni utoro kwa shule za msingi upo kwa asilimia saba na kiwango hicho hicho kwa sekondari.

“Moja ya mambo yanayotukwamisha ni mimba shuleni hali ambayo ni tofauti na mikoa ya wenzetu ya Arusha na Kilimanjaro, lakini utoro ni tatizo lingine ambalo wenzetu chini ya ofisi za wilaya wameliwekea mikakati zaidi,” alisema.

Kwa mara ya pili, Dodoma imeshika nafasi ya 23 katika matokeo ya darasa la saba 2019 licha ya kuongeza ufaulu kwa asilimia nne ukilinganisha na matokeo ya 2018.

Ofisa elimu huyo alitoa pendekezo la kuundwa kwa timu ya kufuatilia maendeleo ya elimu ili kujua lilipo tatizo na kichotakiwa kufanyika kuokoa hali hiyo, jambo lililoungwa mkono na watu wengi na kukubaliana kuanzisha mifuko ya elimu.

Hata hivyo, mbunge wa Chemba, Juma Nkamia alipinga suala hilo wilayani kwake akisema litaleta shida.

Nkamia alisema hawezi kukubaliana na uanzishaji mfuko huo kwa kuwa anaamini hautakuwa na tija, unaweza kuwagawa hata alipoelezwa kuwa wilaya ya Kongwa wameanza na kufikia Sh200 milioni.

Naye katibu tawala mkoa, Maduka Kessy aliwataka wadau kushirikiana na wazazi kukomesha vitendo vya utoro na mimba. Alisema wakati wa kulalamika umepita badala yake wana-Dodoma wanatakiwa kuchukia hali ili kuiondoa Dodoma nafasi za chini

No comments: