Kaimu Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya James Kaji(katikati) akizungumza leo Januari 1, mwaka 2020 jijini Dar es Salaam kuhusu hatua wanazochukua kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya nchini.Pia ameeleza mikakati yao ya kukomesha biashara hiyo haramu nchini
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imesema kuwa imefanikiwa kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya kwa kutoa elimu kwa wazalishaji, wasambazaji wa dawa tiba zenye asili ya kulevya na wafanyabishara wa kemikali bashirifu.
Akizungumza leo Januari 1 mwaka 2020 Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo James Kaji amewaambia waandishi wa habari kuwa wamekuwa na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya na mwaka 2019 wamefanikiwa kudhibiti biashara hiyo kwa zaidi ya asilimia 95 na kazi hiyo inaendelea.
Pia amesema kuwa ili kukomesha bishara ya dawa za kulevya nchini Tanzania, wamefanikiwa kutoa elimu kwa watu wengi kuhusu madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kwamba wengi wameacha kujiingiza kwenye biashara hiyo na wanawachukia wanaojihusisha nayo.
"Wananchi wmakuwa wakisaidia kutoa taarifa kwetu, hali hii imepunguza uwepo wa dawa za kulevya mtaani na watumiaji wanaozagaa hovyo barabarani.Aidha Mamlaka imefanikiwa kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya,"amesema Kaimu Kamishna Jenerali.
Ameongeza pamoja na mafanikio, kumekuwepo na changamoto nyingi katika udhibiti dawa za kulevya ambapo amefafanua kuongezeka kwa udhibitiwa dawa za kulevya kumefanya watumiaji kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya.
Pia wafanyabiashara wa dawa za kulevya wanabuni mbinu mpya kila mara, mfano hivi karibuni Mamlaka imegundua wafanyabishara wa dawa hizo na hasa aina ya mirungi wamekuwa wakisafirisha dawa hizo katika mfumo wa majani makavu, na kuipa majina bandia kama Mronge , Green tea au dawa.
"Kwa mwaka huu tumejipanga kuongeza nguvu katika kujenga vituo vingi ili kuwafikia waathirika wengi zaidi.Tunaendelea kuwakumbusha Watanzania wote kutambua tatizo la dawa za kulevya kuwa ni mtambuka , hivyo tunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla wake kushiriki kwa dhati kabisa katika kukabiliana na tatizo la matumizi na bishara ya dawa za kulevya nchini , hasa kuwafichua wauzaji wa dawa hizo,"amesema.
No comments:
Post a Comment