Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye leo Jumatatu Februari 10, 2020 ametangaza kurejea CCM katika ofisi ndogo za chama hicho tawala nchini Tanzania zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.
Ametangaza uamuzi wake huo mbele ya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally katika kikao cha baraza la wadhamini kilichoanza leo asubuhi. Dk Bashiru ndio mgeni rasmi katika kikao hicho.
Amerejea CCM takribani miezi miwili tangu alipotangaza kuwa si mwanachama wa Chadema.
Desemba 4, 2019 Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu mwaka 1995 hadi 2005 katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alijivua uanachama wa Chadema na kumuachia ujumbe mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe.
Alijiondoa Chadema siku chache baada ya kupigiwa kura 48 za hapana kati ya 76 katika uchaguzi wa uenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani.
Sumaye alieleza kuwa kutokana na yaliyotokea kwenye uchaguzi huo na yeye kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa Chadema akipambana na Mbowe haoni haja ya kubaki katika chama hicho.
Alivyojitoa CCM, kujiunga Ukawa
Agosti 22, 2015 historia iliandikwa katika siasa za Tanzania baada ya Sumaye kujitoa CCM na kujiunga na chama kimojawapo kinachounda Umoja wa Katiba ya Wananchi-(Ukawa).
Ukawa inaundwa na Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF ambacho kwa sasa ni kama hakipo katika umoja huo kutokana na viongozi wake kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo baada ya kurejea kwa Profesa Ibrahim Lipumba. Baadaye Sumaye alichagua kujiunga na Chadema.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu wa zamani wa pili kujiondoa chama tawala katika historia ya Tanzania, ambapo waziri mkuu wa kwanza kuhama CCM na kujiunga na Chadema alikuwa Edward Lowassa, aliyefanya hivyo mwaka 2015. Hata hivyo, Machi Mosi, 2019 Lowassa alirejea CCM.
Sumaye alitangaza uamuzi wa kung’atuka CCM katika mkutano wake na waandishi wa habari akibainisha kuwa amejiunga Ukawa kwa kushirikiana na viongozi wa umoja huo awatumikie Watanzania kwa kasi kubwa baada ya uchaguzi kwa kuwa anaamini Ukawa utashinda.
Amesema kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM na kuvurugwa kwa mchakato wa uchaguzi kumechangia wananchi kukata tamaa hali iliyochochea uungwaji mkono wa upinzani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi
No comments:
Post a Comment