ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 6, 2020

HAKIKISHENI WANANCHI WALIOOKOLEWA KUTOKANA NA MADHARA YA MVUA HAWARUDI MABONDENI TENA: WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Mjaliwa akizungumza na wananchi katika kijiji cha Nambilanje wialyani Ruangwa wakati alipotembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko mkoani Lindi kuwapa pole wananchi, Februari 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi katika kijiji cha Kipindimbi wilayani Kilwa wakati alipotembelea maeneo yaliyoathirika kwa mafuriko katika mkoa wa Lindi, Februari 5, 20-20. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama eneo la mto Njinjo katika kijiji cha Kipindimbi wilayani Kilwa lililoathiriwa mafuriko wakati alipotembelea maeneo yaliyokumbwa na mafuriko katika mkoa wa Lindi, Februri 5, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

NA OWM, LINDI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini wahakikishe wananchi waliokuwa wakiishi mabondeni ambao waliokolewa na kuhamishiwa kwenye maeneo salama hawarejei tena.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Januari 5, 2020) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kipindimbi wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
“…haikubaliki watu waliokuwa wakiishi mabondeni ambao kwa sasa wamehamishiwa kwenye maeneo salama kuona wamerejea tena mabondeni. Wakuu wa Mikoa na Wilaya hakikisheni wananchi hao hawarudi mabondeni.”
Waziri Mkuu amesema Serikali inawataka wananchi hao kutorudi tena mabondeni lengo likiwa ni kuwanusuru na maafa ya mafuriko yanayoweza kujirudia kufuatia mvua kubwa zinazoendele kunyesha nchini.
Amesema Serikali inawajibika kuhakikisha kwamba wananchi wote wanakuwa salama, hivyo ni vyema kuchuwa hatua za kuwaondoa wote waishio mabondeni ili kuwaepusha na maafa yanayoweza kuwapata.
Mbali na kuzungumza na wananchi katika Kijiji hicho cha Kipindimbi, pia Waziri Mkuu ametembelea vijiji vingine vilivyokumbwa na maafa hayo ambavyo ni Nambilanje (Ruangwa), Nakiu na Njinjo (Kilwa) na Kitomanga (Lindi) ili kujionea athari za mafuriko na kuwapa pole wananchi.
"Naomba mpokee salamu za pole ninazozileta kwenu kutoka kwa Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa kwa wananchi wote waliokumbwa na mafuriko hayo kwa kupoteza ndugu zetu wapendwa pamoja na mali."
Awali,Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema mvua hizo zilizonyesha mfululizo zilisababisha maafa makubwa ambapo watu 21 walifariki huku wengine 26,481 katika kaya 4,344 wakikosa makazi.
Bw. Zambi alisema kuwa mbali na kusababisha vifo pia maeneo mbalimbali ya kutolea huduma nayo yameathirika. Maeneo hayo ni pamoja na shule, zahanati, miundombinu ya barabara, maji na mashamba ambayo yamefunikwa na maji.
“Mvua hizi zilisambaa katika wilaya zote za Mkoa wa Lindi, hata hivyo athari kubwa zilitokea kwenye wilaya za Kilwa kata zilizoathirika ni saba, Ruangwa kata 18, Liwale kata tatu na Lindi kata nne.”
Mkuu huyo wa mkoa alisema mkoa wa Lindi ulikumbwa na maafa ya mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha Januari 18 na 19 na ziliongezeka zaidi Januari 23 hadi 29, 2020.
Alisema kutokana na nyumba nyingi kuzingirwa na maji au kubomoka shughuli za uokoaji zilifanyika katika maeneo hayo ambapo watu waliookolewa walihifadhiwa katika kambi za muda za uokoaji zilizofunguliwa katika maeneo mbalimbali.
Alisema mkoa umepokea misaada mbalimbali ikiwemo ya kutoka kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Mafaa ambayo imetoa mahema 80, mablanketi 50, ndoo 1,500, mikeka 350 pamoja na vikombe 350. “Pia tumepokea misaada ya vyakula, nguo, dawa na vifaa vya shule kutoka kwa wadau mbalimbali.”
Mkuu huyo wa mkoa aliongeza kuwa walipokea vifaa vya uokoaji zikiwemo boti nane kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), TFS, Halmashauri na watu binafsi, Helikopta mbili kutoka JWTZ na Jeshi la Polisi na mitumbwi saba kutoka kwa watu binafsi.

No comments: