ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 13, 2020

NAIBU BALOZI WA ISRAEL NCHINI ATEMBELEA TAASISI YA JKCI

Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David ameuomba uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa ushirikiano kwa madaktari wa Israel watakaotembelea taasisi hiyo hivi karibuni ili kwa pamoja waweze kuainisha mahitaji yaliyopo katika kuboresha huduma za matibabu ya moyo.
Akizungumza na wajumbe wa menejimenti wa JKCI leo Jijini Dar es Salaam naibu balozi Mhe. Eyal alisema ushirikiano ulioanzishwa na nchi hizo mbili tangu mwaka 1998 umekuwa wa mafanikio makubwa katika kuokoa maisha ya watoto wenye magonjwa ya moyo hapa nchini.
“Madaktari kutoka nchini Israel waliopo katika hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma watatembelea hapa, ninawaomba mtoe ushirikiano kwao na kuwaonesha maeneo mbalimbali ya taasisi ili kwa pamoja muweze kuainisha mahitaji yaliyopo nasi tutayapitia na kuona namna gani tunaweza kusaidia”, alisema Mhe. Eyal.
Naibu Balozi Eyal aliendelea kusema Israel imekua ikijivunia kuwekeza katika utoaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na kuahidi kuendelea kushirikiana na JKCI ili kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi wenye matatizo ya moyo.
“Tunajivunia kuwekeza katika utoaji wa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto nchini Tanzania kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete. NInaaminii ushirikiano huu utaendelea na kuleta mafanikio makubwa zaidi katika utoaji wa matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto”, alisema Naibu Balozi Eyal.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alimshukuru Naibu Balozi huyo kwa kuwa sehemu ya kuendeleza ushirikiano na kuomba mafunzo yanayotolewa na Israel kwa wafanyakazi wa Tasisi hiyo yaguse pia na kwa wafanyakazi ambao siyo wa kada ya afya.
“Serikali ya Israel imekuwa ikitoa mafunzo mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wauguzi na madaktari lakini kwa sasa ninaomba pia mtoe mafunzo kwa wafanyakazi wa kada nyingine zilizopo katika Taasisi yetu”, alilisisitiza Prof. Janabi.
Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David akimjulia hali mtoto Nickson Tarimo aliyefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati alipotembelea Taasisi hiyo leo akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma.
Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David akimpa pole mtoto Andrew Mwanawima aliyelazwa katika wodi ya watoto ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Mhe. Balozi David alitembelea Taasisi hiyo leo akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimwelezea Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David namna ambavyo Taasisi hiyo inavyoshirikiana na Israel kupitia taasisi ya Save a Child’s Heart (SACH).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimwonesha Naibu Balozi wa Israel nchini mwenye makazi yake Jijini Nairobi nchini Kenya Mhe. Eyal David picha za wajumbe wa kwanza wa bodi ya wadhamini pamoja na menejimenti ya kwanza ya Taasisi hiyo wakati balozi huyo alipotembelea JKCI leo akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma.
Picha na: Genofeva Matemu - JKCI

No comments: