ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 29, 2020

ANTI BETTIE: Mwaka wa nne sasa sijaonana naye, ila bado anasisitiza nivumilie

Kuna mwanamke nampenda na anavyodai yeye ananipenda. Huu ni mwaka wa nne ameondoka kwa madai ya kwenda kusoma, hajawahi kurudi likizo hata moja na nikitaka kuzungumza naye kwa njia ya simu hadi nimuanze, lakini ananihakikishia bado ananipenda niendelee kusubiri.

Nifanyeje?

Umesema hata simu lazima umuanze, ina maana hata kukuambia anakupenda hajakwambia, kuendelea kuvumilia pia ni kama unamlazimisha. Mtu anayekupenda hata kama ana maisha au mazingira magumu kiasi gani hawezi kukaa mbali nawe kwa miaka minne na hata simu zake ziwe za kulazimisha.

Ninachokiona hapo ni kama unapoteza muda kumsubiri mtu asiyekufikiria, unachotakiwa kufanya ni kumpima kama kweli ana nia ya dhati na wewe. Usimpigie simu, uone atakaa kimya mpaka lini yaani bila kukutafuta, hapo utapata jibu kama ana nia na wewe au anakupotezea muda. Hujasema kama una kazi au shughuli ya kukuingizia kipato, ila kama unayo na una fedha kidogo unaweza pia kujiridhisha kwa kwenda huko anakosema anasoma, bila shaka ni hapa nchini.

Kama anakupenda atakuruhusu kwenda, iwapo anakupotezea muda atakuambia usijali ngoja amalize mtaonana tu.

Ikitokea akakuruhusu uende hali utakayoikuta huko pia itakupa jibu la maswali yako, maana hatataka muongozane kila mahali, hatakutambulisha kwa rafiki zake na kila mara atakuwa anakupigia hadithi za kuondoka kwako hata kabla hujaaga.

Aliniacha, akaoa sasa anataka turudiane ?

Anti habari!

Nilifunga ndoa na kupata mtoto mmoja na mume wangu. Mtoto alipofikisha miezi mitatu nilimuomba nikasalimie nyumbani. Nikiwa nyumbani alinipigia simu na kunieleza nibaki huko huko akidai ameshaoa, nikamjibu sawa sasa ananisumbua anataka turudiane.

Nifanyeje?

Kwanza hujanielewesha vizuri, kama alikuoa alikuachaje kienyeji namna hiyo na wewe ukakaa kimya bila kuchukua hatua yoyote? Kwa uelewa wangu ulipaswa uwafahamishe wazazi wako au wakwe zako ambao wangewasiliana na mtoto wao kujua hatma ya ndoa yenu. Kama ni kweli amekufanyia hivyo, ina maana hakuwa makini na ndoa yake na hana adabu hata kidogo.

Angekua na adabu asingekutamkia au kufanya kitendo cha kifedhuli kiasi hicho. Unachotakiwa kufanya ni kuwataarifu wazazi wako kwa nini upo nyumbani kwa kipindi chote ulichokaa.

Kisha uende kwa wakwe zako ukawafahamishe na uwaeleze anachokitaka mtoto wao kwa wakati huo. Lakini weka angalizo kuwa hutamsamehe hadi ajieleze kwa wazazi wa pande zote mbili kwa sababu aliwadharau.

hata wao, kwa kitendo alichokifanya na aape kuwa hatarudia.

Muhimu, kama mtapatanishwa kwa sababu kikao cha familia hakivunji ndoa, sharti lako la kwanza liwe kwenda kupima kwa ajili ya kuangalia afya zenu, kwa sababu mwenzako alishaanzisha uhusiano na mtu mwingine, ikiwezekana mpime kwa miezi yote mitatu kabla ya kuendelea na maisha kama kawaida.

Kama mmepanga usikubali kurudi katika nyumba uliyokuwa ukiishi naye na baadaye akaja kuishi na mwanamke mwingine, ufuatilie pia kama alifunga ndoa ni ya aina gani na imevunjwa au laa, usije kuishi na mwanaume mwenye ndoa nyingine mahali.

Usisahau kuishi naye kwa tahadhari kutokana na alichokufanyia hapo awali.

No comments: