ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 30, 2020

TUTATUE MATATIZO YETU KWA KUANGALIA HALI ZETU.

*Tupambane na hali zetu, tujikune tunapoweza kupafikia!*

- Unawawekaje watu nyumbani hawana mafriji ya kuhifadhia chakula?

- Unawawekaje nyumbani watu wanaonunua sukari robo na unga nusu kilo?

- Unawawekaje nyumbani watu wanaoununua umeme wa luku?

- Unawawekaje nyumbani watu wanaochota maji bombani? Muuza maji wao ya debe pia utamzuia asitoke ?

- Unawawekaje nyumbani watu wanaotumia simu za vocha?


- Unawawekaje nyumba
ni watu wanaoishi nyumba ya vyumba sita familia sita? Mlango wa mbele hauna umuhimu, labda usiku ndio unageresha geresha umefungwa. Si wataambukizana humo humo ndani ya nyumba, si bora watoke nje?

- Unawawekaje nyumbani watu ambao hawawezi kufanya kazi kwa kompyuta wakiwa nyumbani? Umachinga unawezekana kufanyika online?

- Unawawekaje nyumbani watu ambao hawawezi kuoda chakula online kama walivyofanya China?

- Unawawekaje nyumbani watu ambao wakikosa kazi hawalipwi mshahara. China, Italy kuna mafao kwa wanaokosa kazi. Ulaya yote na Marekani ni hivyo hivyo. New York wasio na kazi wanalipwa dola 700 kwa wiki. Meya wao kaongeza dola 600 za corona. Mtu anakaa nyumbani analipwa dola 1300 kwa wiki. Sio deni wala mkopo. Na mkewe pia anapata hizo hizo.

- Unawawekaje nyumbani watu ambao serikali haiwezi hata kuwaingizia pesa kwenye akaunti zao wala kuwatumia cheki za pesa za msaada? Watatumia anuani zipi?

Watu wafuate masharti ya wataalamu, *MIPAKA, BANDARI/FORODHA NA VIWANJA VYA NDEGE VIFUNGWE KISAWASAWA* Hata Marekani wamesalimu amri jana. Ndege za Ulaya zimeacha kuja Marekani.

Watu wapunguze mikusanyiko isiyo ya lazima. Wanaoweza kufanya kazi wakiwa nyumbani wafanye hivyo. Karantini ipewe umuhimu wa hali ya hatari, hata ikibidi watu wafungwe jela. Kwa kuangalia video za China nimegundua watu wakitishiwa jela wanaelewa haraka kuliko kuchapwa viboko.

Kwa Washington DC wanafunzi wa shule za msingi walipewa homework. Na kuanzia kesho wataanza masomo kwa njia ya mtandao. Mwaka wao wa shule umebaki miezi miwili tu.
Kwa Tanzania kama shule zitafungwa kwa muda mrefu ni bora kuangalia uwezekano wa kufundisha kwa kutumia televisheni kama ni vigumu kufundisha wanafunzi mtandaoni.

Zaidi yao hayo kila mtu aombe kwa dini yake na Mungu wake hali isifikie kuwa mbaya kama Ulaya, China na Marekani. Kuna video inatembea Facebook inaonyesha mochuari moja ya New York imejaa, maiti zinawekwa kwenye malori yenye mafriza.

Watu wachape kazi, miradi iendelee. Tanzania iendelee kama Marekani na China. Ikumbukwe si mbali, ni mwaka 1980 tu, China ilikuwa ni nchi maskini sana.

Mungu ibariki Tanzania.

No comments: