Kiungo nyota na nahodha wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi jana alikuwa na kikao kizito na vigogo wa GSM kuhusiana na hatma yake ambapo leo atasaini mkataba mpya wa miaka miwili.
Mwanaspoti lilimshuhudia mchezaji huyo akiingia kwenye ofisi za GSM Jijini Dar es Salaam na kukaa kwa muda wa saa 1:10 na alipotoka akaonyesha dole gumba akimaanisha ishu zinakwenda freshi.
Mmoja wa vigogo wa GSM alisema jana kwamba wameshakubaliana mambo mengi na mchezaji huyo na atasalia Yanga na hata wao wamerejea kama ilivyokuwa awali ndio maana wanaendelea na mchakato wa kuisuka Yanga.
Aliongeza pia kwamba kama mambo yatakwenda vizuri baina yao na wakala, huenda Heritier Makambo ‘Mzee wa kuwajaza’ akarejea Jangwani akitokea AC Horoya ya Guinea, ambako mambo hayajamuendea poa.
Katika hatua nyingine benchi la ufundi la Yanga, limepanga kuisuka timu hiyo kivingine na tayari Mwanaspoti imenasa silaha tano mpya wanazoanza nazo.
Habari za uhakika zinasema kwamba kocha Luc Eymael amepanga kuanza kwa kufumua safu ya ulinzi na pia ya umaliziaji. Lakini mashabiki wanaweza kukumbwa na mshtuko kwani Mbelgiji huyo amepanga kumpiga chini beki mzoefu Kelvin Yondani kwa kigezo cha kiwango, umri pamoja na nidhamu.
Ngoja tukupe kwanza listi yake mpya. Luc amepanga kumshusha Jangwani kipa namba moja wa KMC, Jonathan Nahimana ambaye ni raia wa Burundi.
Katika mechi ambayo KMC iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Nahimana alikuwa kikwazo kwa washambuliaji wa Yanga kupata mabao na alionyesha ukomavu uliomfanya kocha Eymael kuondoka na jina lake kama mbadala wa Farouk Shikhalo ambaye ni Mkenya.
Usajili mwingine ni wa beki wa kulia wa KMC, Kelvin Kajiri ambaye katika mechi dhidi ya Yanga alionyesha kiwango kizuri na kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga licha ya mshambualiaji Salum Kabunda kushindwa kuzitumia.
Kocha Eymael anaona Kajiri ni mbadala sahihi wa Juma Abdul huku Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye alikuwa majeruhi muda mrefu atakuwa anacheza nafasi nyingine.
Habari zinasema kwamba mbali na mastaa hao ambao hawana majina makubwa, Yanga pia itashusha kombora kwenye klabu ya Namungo kwa kuwanyakua juu kwa juu, Reliants Lusajo, Bigirimana Blaise ambao ni washambuliaji na beki Minza Bale.
Habari za ndani zinasema kwamba Mbelgiji huyo anapanga kufanya mabadiliko makubwa na amepania kuwachukua wachezaji hao watano kwa kigezo cha umri pamoja na ufanisi wao uwanjani.
Mwanaspoti limeambiwa kwamba majina hayo yapo kwa wajumbe wa kamati ya ufundi pamoja na benchi la ufundi ambapo muda mfupi ujao watakabidhi rasmi kwa GSM na uongozi tayari kumalizana na mastaa hao na anataka hilo lifanyike mapema kabla ya ishu za usajili hazijaanza rasmi kwani mastaa hao wanauzika.
Chanzo chetu kimesema kuwa Minza anachukuliwa kama mbadala wa Jafari Mohamed ambaye anacheza nafasi ya beki wa kushoto Yanga huku Lusajo na Blaise wataimarisha nafasi ya ushambuliaji.
Lusajo kwa sasa amefunga mabao 11 akiwa katika nafasi ya pili pamoja na Paul Nonga wa Lipuli na Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar ya huku mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere akiongoza kwa kufunga mabao 19.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo, kocha Eymael alisema ni mapema sana kutangaza majina ya wachezaji ambao watasajiliwa au kuachwa.
“Hii ni siri ya klabu, mimi nawajibika kwa viongozi ambao nawapa mapendekezo yangu,” alisema Eymael ambaye yupo kwao Ubelgiji kwa mapumziko ya muda mfupi na hawezi kurejea nchini mpaka mipaka ya nchi yao ifunguliwe Serikali yao itakapojiridhisha kwamba Corona imepoa.
No comments:
Post a Comment