Thursday, April 2, 2020

MSISUBIRI SERIKALI ISEME, PANDENI MITI-RC MWANGELA

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akipanda mti katika chanzo cha maji cha Ilolo Wilayani Mbozi katika maadhimisho ya Siku ya kitaifa ya Upandaji miti ambapo kimkoa yamefanyika Wilayani Mbozi kwa viongozi na Baadhi ya wananchi kupanda miti.
Miti aina mizambarau pori iliyopandwa katika chanzo cha maji cha Ilolo Wilayani Mbozi katika maadhimisho ya Siku ya kitaifa ya Upandaji miti ambapo kwa Mkoa wa Songwe wananchi wamehimizwa kupanda miti bila kusubiria maelekezo ya serikali.
Wananchi wa Wilaya ya Mbozi Wakishiriki zoezi la Kupanda miti katika chanzo cha maji cha Ilolo Wilayani Mbozi katika maadhimisho ya Siku ya kitaifa ya Upandaji miti ambapo kimkoa yamefanyika Wilayani Mbozi kwa viongozi na Baadhi ya wananchi kupanda miti.

NA MWANDISHI WETU, SONGWE.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ametoa rai kwa wananchi wote kujenga mazoea ya kupanda miti bila kusubiri maagizo au maelekezo kutoka serikalini ya kuwataka kufanya hivyo.
Brig. Jen. Mwangela ametoa rai hiyo mapema leo katika chanzo cha maji cha Ilolo Wilayani Mbozi wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya Upandaji Miti ambapo kwa Mkoa wa Songwe maadhimisho hayo yamefanyika kwa viongozi mbalimbali kupanda miti.
Amesema wananchi wajenge tabia ya kupanda miti kwa wingi kwakuwa miti ina faida nyingi na pia Mkoa wa Songwe una ardhi nzuri ambayo inawezesha aina nyingi za miti kustawi.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa licha ya Mkoa wa Songwe kuwa na hali ya hewa nzuri, kipaumbele kiwe ni kupanda miti kwa wingi kwakuwa isipo fanyika hivyo itafikia kipindi mvua zinazo patikana hivi sasa hazitakuwepo.
Aidha ameziagiza halmashauri za Wilaya kuhakikisha zinatunza vizuri vyanzo vya maji na mikakati inawekwa ya kuhakikisha miti inayopandwa yote inakua vizuri ikiwa ni pamoja na kutorusu mifugo kusambaa na kuharibu vyanzo vya maji.
Afisa Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Charles Ndimbo amesema kwa sasa wanaendelea kuwahamasisha wananchi kujengea wigo katika maeneno yote waliyopanda miti na kuzuia mifugo yao isizurure na kufanya uharibifu.
Ndimbo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi inasimamia misitu 70 huku Lengo likiwa ni kupanda miti milioni mbili kwa Mwaka Lakini kwa mwaka 2018/2019 zaidi ya miti milioni 1.6 ilipandwa huku iliyofanikiwa kukua ikiwa ni miti milioni 1.1.
Amesema kuna sababu mbalimbali zinazopelekea miti inayopandwa kushindwa kukua ikiwa ni pamoja na miti hiyo kupandwa katika maeneo yasiyo faa, kuliwa na wadudu, kuharibiwa na mifugo, ukame pamoja na kuchomwa moto.
Nao baadhi ya wananchi walioshiriki maadhimisho ya siku ya upandaji miti wameiomba serikali kuendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wanao haribu miti.
Kaulimbiu ya kitaifa ya maadhimisho ya Siku ya Upandaji miti kwa mwaka 2020 ni, “Tutunze Mazingira, tukabiliane na Mabadiliko ya tabia Nchi”

No comments: