Thursday, April 2, 2020

Ndugai Akataa Hotuba ya Upinzani Kusomwa Bungeni

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanzania, Job Ndugai, amezuia kusomwa kwa hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kuhusu hotuba ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kwa sababu imekiuka kanuni za Bunge.

Hotuba hiyo ilikuwa isomwe jana Jumatano Aprili Mosi 2020 na Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Bungeni, Freeman Mbowe. Akizungumza kabla ya Mdee kuruhusiwa kuisoma, Ndugai alisema baadhi ya mambo yaliyoandikwa katika hotuba hiyo ni ya uzushi.

Amesema taarifa kuwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu analidai Bunge ni za uzushi na kwamba hakuna mbunge anayedai.

Ndugai aliongeza kwamba ndani ya hotuba hiyo kuna madai kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani hapati huduma ambapo alijibu kwamba Mbowe analo gari na kwamba kama kuna tatizo kama la ubovu, ni jambo la kuwasiliana na Katibu wa Bunge.

Aidha, alisema Mbowe anayo nyumba ambayo aliikataa na badala yake alimpatia mnadhimu wa kambi rasmi ya Bunge (wakati huo Lissu) na yeye kuishi kwenye nyumba yake binafsi. Hata hivyo, amesema Bunge halitoi nyumba kwa mnadhimu wa kambi ya upinzani.

Ndugai alisema ingawa Mbowe alikataa nyumba hiyo lakini amekuwa akipata huduma zote anazostahili kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani ikiwemo ulinzi, mhudumu, maji na nyingine anazostahili.

“Anasema hajapewa wasaidizi lakini tuliwaondoa wasaidizi wote hata wa CCM tuliwakataa kwa sababu ya usalama,” amesema.

Alisema ofisini ana wasaidizi wanne ambao ni katibu muhtasi, mhudumu, ofisa mwandamizi na dereva. Awali, Ndugai alikuwa akiwaruhusu kusoma bajeti kwa kuondoa baadhi ya maeneo lakini hivi sasa hataruhusu kusomwa tena hotuba za namna hiyo.

No comments: