ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 5, 2020

Wauguzi 15 wa saratani wapata corona nchini Misri

Cairo, Misri. Wafanyakazi 15 wa afya katika Hospitali kuu ya saratani ya Misri wamegundulika kuambukizwa virusi vya corona.

Aidha, watumishi hao kwa sasa wanapatiwa matibabu ambako watalazimika kukaa karantini kwa muda wa wiki mbili mpaka watakapopimwa tena.

Meneja wa Taasisi ya taifa ya saratani iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Cairo, Dk Reem Emad alisema jana kuwa wafanyakazi hao ni madaktari watatu na wauguzi 12.

Msemaji wa Chuo Kikuu cha Cairo, Mahmoud Alameldeen alisema kutokana na watumishi hao kuugua sasa taasisi hiyo itawapokea wagonjwa wa dharura pekee.

“Tunaomba wagonjwa ambao si wa dharura wasije kwa sasa katika hospitali yetu kutokana na watumishi wengi kuwekwa karantini hivyo shughuli nyingi zimesimama,” alisema Alameldeen.

Wizara ya Afya ya Misri ilisema mpaka jana asubuhi nchi hiyo ilikuwa na wagonjwa wa corona 985.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, watu 66 wamepoteza maisha tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kuingia mwezi Februari.

Serikali ya Misri imepiga marufuku ya wiki mbili ya kutotoka nje kuanzia Machi 25, ili kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo.

Shule, vyuo, kumbi za starehe, makanisa na misikiti vyote vimefungwa katika nchi hiyo.

Zaidi ya watu 1,153,287 wamethibitishwa kuathirika na virusi vya corona duniani.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), vifo vilivyotokana na maambukizi ya corona hadi jana jioni vilikuwa ni watu 61,663. Pia, ripoti za shirika hilo zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 240,000 wametibiwa na kupona virusi hivyo.

Ripoti hiyo inaonyesha Marekani inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Covid-19.

Ripoti hiyo inasema hadi jana nchi hiyo ilithibitisha kuwa na zaidi ya waathirika 290,000 na vifo 7,844 ikifuatiwa na Hispania yenye wagonjwa 124,000.

Hata hivyo, nchi inayoongoza kwa kuwa na vifo vingi vilivyotokana na virusi vya corona ni Italia ambako mpaka jana zaidi ya watu 14,681 waliripotiwa kufariki dunia.

Ugonjwa huu wa Covid-19, uliibuka kwa mara ya kwanza nchini China Desemba, 2019 katika mji wa Wuhan na kusambaa katika nchi zaidi ya 150 duniani.

Mpaka sasa Marekani imeweka rekodi ya kuwa na vifo vingi vinavyotokana na virusi hivyo kwa siku moja.

Alhamisi iliyopita chi hiyo ilithibitisha kupoteza zaidi ya watu 1,000 katika kipindi cha saa 24 idadi ambayo iliipiku Hispania ambayo kwa siku hiyo ilipoteza watu 950.

Idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa corona Hispania iliyoweka rekodi ya kuwa taifa la pili kuwa na maambukizi mengi ilipanda kutoka 102,136 Jumatano iliyopita na kufikia 110,238 kwa jana asubuhi.

No comments: