MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM, Mtanzania
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amedai wabunge wengi wa upinzani ambao katika Bunge la 11 walipewa adhabu mara nyingi bungeni ni watumiaji wa dawa za kulevya, wavutaji wa bangi na wanywaji wa pombe kali.
Alisema ndio maana wengi wa wabunge wa aina hiyo wamekuwa na tabia mbaya kupitiliza, ambapo wamekuwa wakiropoka ovyo na kutukana kwa sababu akili inakuwa si yao.
Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, alitoa madai hayo wakati akihojiwa na Kipindi cha 360 cha Clouds TV nyumbani kwake jijini Dodoma jana. Ndugai alisema Bunge la 11 ambalo wiki iliyopita lilivjwa na Rais John Magufuli ili kupisha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, vitendo vya utovu wa nidhamu vilikithiri.
Pia alikiri miongoni mwa mapungufu makubwa katika Bunge lake hilo, ni kitendo cha Bunge kutorushwa moja kwa moja live.
“Na wengi wakorofi ambao mara nyingi wamekuwa wakipewa adhabu ni watumiaji wa dawa za kulevya, wavutaji bangi na wanakunywa pombe kali, ndio maana wanafika pale wanajiropokea tu, akili inakuwa sio yao.
“Baada ya wabunge wanaofanya makosa kuadhibiwa, vyombo vya habari vimekuwa vikiwabeba kwa kutoa taarifa zao.
“Tulisema mwaka mzima itakuwa adhabu kubwa lakini hata akienda huko (mbunge ) anatamba, ni shida sana na watu kama hawa wanaonekana kwa vijana kama mashujaa.
“Vyombo vya habari na mitandao inakuza watu wa ovyo. Wasema ovyo na waropokaji wanafanywa kuwa mashujaa,”alisema Ndugai.
Alisema changamoto hiyo inatakiwa itafutiwe ufumbuzi ili isijitokeze katika Bunge la 12 linalotarajiwa kuanza Novemba mwaka huu.
Alishauri ili changamoto hiyo imalizike, inatakiwa wananchi wasiwarudishe bungeni wabunge wenye tabia hizo na vyombo vya habari kuacha kutoa taarifa zao.
“Kuendelea kurusha taarifa za wabunge hao si sawa, ndio maana tunahitaji msaada wa vyombo vya habari, tunapoelekea Bunge la 12. Naamini wapiga kura watachuja walio wengi katika hawa.”
“Ukiacha uropokaji wao (wabunge anaodai ni walevi, watumia madawa) bungeni, hakuna walichofanya, wao ni kuropoka na kulaumu, lakini hakuna cha maendeleo walichofanya majimboni kwao,”alisema Ndugai.
BUNGE LIVE
Katika hatua nyingine, Ndugai alisema sababu kubwa ya matangazo ya bunge kutorushwa moja kwa moja, ni kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu katika Bunge.
Alisema baadhi ya wabunge aliowaita waropokaji, walikuwa wakiona kamera wanabadilika na kuropoka lakini kamera zikiwa hazipo wanazungumza inavyopaswa.
“Tukafika mahali ambapo live camera ikaliharibu Bunge, watu wakawa wanatukana, wana tabia mbaya, unakuta mmekubaliana kwenye kanuni kuwe na nidhamu, lakini watu wanabadilika wanacheza mchezo wa kuigiza.
“Wanacheza na wananchi kupotosha kila kitu, tuwaza kwanini mtu kamera ikiwa haipo anafikiri sawasawa, ikiwa ipo anabadilika, ni moja ya sababu iliyofanya tuangalie ni nini cha kufanya,”alisema.
Wakati Ndugai akisema hivyo jana, wakati mfumo wa Bunge live ukiondolewa, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo, Nape Nnauye, alisema hatua hizo zinachukuliwa ili kupunguza gharama za kurusha vikao vya mubashara. Nape alisema pia kitendo cha Bunge kuonyeshwa live, kiliwafanya wananchi kutofanya kazi na kubaki wakifuatilia Bunge.
SHERIA VYOMBO VYA HABARI
Katika mahojiano ya jana, Ndugai alipoulizwa kuhusu namna sheria ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 inavyowabana waandishi wa habari, alisema ni kweli vyombo vya habari vimebanwa na sheria hiyo.
“Tuwe wa wazi tu, ni kweli sheria ile imebana vyombo vya habari, wakati tunaiandaa ukimwuliza mbunge yeyote wa chama tawala atakwambia kibano kile hakitoshi kwa sababu media (vyombo vya habari) zinawabeba wenye tabia mbaya ya kupitiliza.
“Kwanza ukiangalia tu lile kundi la wabunge wa upinzani hasa viongozi ambao wanakaa pale mbele jinsi walivyo tatizo kuanzia tabia zao, walio wengi wamekunja mikono lakini kundi la wachache wao ndio wanasema kila siku, demokrasa hakuna ni kuoneana tu.
“Sasa matokeo yake mtayaona baada ya uchaguzi, kambi ile itapungua kwa sababu wametumia nafasi vibaya,”alisema Spika Ndugai.
No comments:
Post a Comment