ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 20, 2020

Simba yaipiga Mwadui kibabe

BAADA ya kutoka sare katika mchezo wao uliopita dhidi ya Ruvu Shooting, hatimaye kikosi cha Simba kimeibuka na ushindi wao wa kwanza leo dhidi ya Mwadui, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam tangu kurejea kwa Ligi Kuu Bara, Juni 13.

Ligi Kuu Tanzania Bara ilisitishwa Machi 17 kutokana na janga la virusi vya corona huku Simba wakiwa vinara wa Ligi hiyo, wakiwa na pointi 71 kabla ya kurejea na kuvuna pointi nne katika michezo miwili waliyocheza.

Katika mchezo wa leo, Simba wameishushia kipigo Mwadui cha mabao 3-0 huku wakicheza soka la kuvutia tofauti na ilivyokuwa katika mchezo wao wa kwanza ambapo walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Ruvu Shooting.

Mabao ya Simba, mawili yalifungwa kipindi cha kwanza na Hassan Dilunga huku la pili beki wa Mwadui, Augustino Samson akijifunga baada ya kupigwa kwa pasi mpenyezo na Shomary Kapombe aliyepanda kushambulia.

Bao la tatu la Simba, lilifungwa na nahodha wa kikosi hicho, John Bocco baada ya shuti la Luis Miquissone kugonga nguzo na kumalizia kwa kichwa mpira ulioshiwa kutazamwa na kipa wa Mwadui, Mahmoud Amir.

Baada ya kupata mabao hayo matatu, Simba walifanya mabadiliko kwa kuwatoa, Bocco,Fraga,Kapombe, Dilunga na Luis nafasi zao wakaingia, Meddie Kagere, Francis Kahata, Cletous Chama, Yusuf Mlipili na Mzamiru Yassin.

Chama ambaye mchezo wa leo ulikuwa wa kwanza kwake tangu arejee nchini akitokea kwao nchini Zambia alionekana kuwakosha mashabiki wa Simba kutokana na mbwembwe za hapa na pale ambazo alikuwa akizifanya.

 Mwanaspoti


No comments: