ANGALIA LIVE NEWS
Monday, July 13, 2020
JPM awaunganisha Diamond, Kiba, Harmonize
CHRISTOPHER MSEKENA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli, amefanikiwa kuwaweka pamoja mahasimu wakubwa kwenye muziki, Diamond Platnumz, Ali Kiba na Harmonize katika hafla ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kutembelea ujenzi wa Ofisi za Ikulu, Chamwino jijini Dodoma, jana.
Diamond, Ali Kiba, Harmonize walilazimika kuweka tofauti zao pembeni na kukaa meza moja huku wakiongoza jopo la wasanii waliotoa burudani katika hafla hiyo iliyohudhuliwa na maelfu ya wanachama wa CCM.
Wakati akimalizia hotuba yake, Rais Magufuli aliwashukuru wasanii mbalimbali walioshiriki kwenye hafla hiyo huku akiwapongeza mahasimu hao kwa kukaa pamoja.
“Ukiona Ali Kiba anakaa pamoja na Diamond hapo ndio unaiona nguvu ya CCM au ukimuona Harmonize aliyemkimbia Diamond leo anamsifia hadharani hapa inapendeza kweli, hii ndio Tanzania tunayoitaka, mimi shabiki yenu nawafuatilia sana,” alisema Rais Magufuli.
Kwa miaka zaidi ya saba sasa Diamond na Kiba wamekuwa hawaivi chungu kimoja na uhasimu wao unatajwa kama moja ya bifu lenye nguvu zaidi kuwahi kutokea kwenye Bongo Fleva huku Harmonize akiwa kwenye uadui mkubwa na mashabiki wa Diamond baada ya kujitoa kwenye lebo ya WCB.
Aidha Rais Magufuli alisema anafahamu ana deni kubwa kwa wasanii kuhusu kubadili shughuli za sanaa kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya COSOTA kuja kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.
“Sanaa imesota sana huko, nawaahidi wasanii kabla ya kufika Jumapili inayofuata haya yote nitayamaliza, Waziri Mwakyembe nataka kabla haujaenda kuchukua fomu kule kwenu uje uchukue barua nitakayokuwa nimeisaini ya kuhamisha shughuli za COSOTA kutoka kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara kuja kwenye Wizara yako ili hawa vijana wafaidike na usanii wao,” alisema Rais Magufuli.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment