Thursday, August 6, 2020

Dkt. Abbasi: Nimeridhishwa na viwanja vya wachezaji ni vizuri


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi (aliyeshikilia karatasi lenye ramani ya viwanja) akiwa eneo la Mtuma kukagua  viwanja vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt John Pombe Magufuli kwa  wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) leo Agosti 6,2020 jijini Dodoma.


Na Eleuteri Mangi, WHUSM-Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amefanya ziara  ya kukagua  viwanja vilivyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt John Pombe Magufuli kwa  wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars).

Katibu Mkuu amefanya ziara hiyo leo eneo la Mtumba jijini Dodoma ili kukagua na kujionea viwanja vilivyotolewa na Rais kabla ya kukabidhiwa kwa wachezaji na viongozi wao.

“Leo tumetembelea na kufanya ukaguzi wa mwisho wa viwanja vya makazi ambavyo Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivitoa kwa wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilifuzu na hatimaye kushiriki michuano ya Fainali za Afrika baada ya miaka 40” 

Akiridhishwa na kazi iliyofanywa na wachezaji hao, Mwaka jana 2019 Mhe. Rais Dkt. Magufuli alitoa viwanja vya makazi Machi 25, 2019 Ikulu jijini Dar es salaam kama zawadi yake kwa niaba ya watanzania kwa wachezaji wa timu ya Taifa Stars, Benchi la ufundi, wachezaji wa zamani Peter Tino, Leordiga Tenga, Bondia Hassan Mwakinyo na kocha wake. 

Dkt. Abbasi amesema kuwa kutolewa kwa viwanja hivyo vya makazi na Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli viwe chachu kwa wanamichezo, vijana, vyama vya michezo na mashirikisho hatua inayosaidia kuhakikisha mipango mbalimbali ya michezo ndani na nje ya nchi wanaitekeleza kwa kushirikisha Serikali ili kuongeza tija katika michezo hiyo.

Mchakato wa kupata viwanja hivyvya makazi o umefanyika na hatimaye umekamilika vipo eneo la Mtumba Jijini Dodoma mbele kidogo ya mji wa Serikali, barabara ya kuelekea Chamwino Ikulu na barabara kuu ya Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Dkt. Abbasi amesema kuwa ofisi yake imejiridhisha viwanja vilivyotolewa na Mhe. Rais ni vizuri na vina ukubwa kati ya mita za mraba 1200 hadi 2300 na zoezi la kukabidhi viwanja hivyo kwa wahusika wote litafanyika hivi karibuni.

Aidha, Serikali inawajali wanamichezo na kuna mambo mengi yanayofanya ili kufanikisha mikakati ya kukuza sekta ya michezo nchini ikiwemo kuwapa zawadi wachezaji wa michezo mbalimbali wanapofanya vizuri.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake