Thursday, August 6, 2020

WAFANYAKAZI 70 WAACHISHWA KAZI KAMPUNI YA MANTRA

NA  YEREMIAS  NGERANGERA, NAMTUMBO

Kampuni ya  Mantra Tanzania  limited  iliyotegemewa  kuanzisha  mgodi wa uchimbaji wa madini ya Urani  katika kijiji cha Likuyusekamaganga  wilayani  Namtumbo  Mkoani Ruvuma  imepunguza wafanyakazi  70  kutokana  na mgodi kutoanza  kufanya kazi  ya uchimbaji.

Akiongea  akiwa shule ya Msingi Mwenge  katika mamlaka ya  mji mdogo wa Namtumbo  Afisa  Mahusiano wa kampuni  ya Mantra  Tanzania  limited BI. Adija Pallangyo  alisema Kampuni ya Mantra imepunguza  wafanyakazi wake  kutoka  84 mwaka 2014 na kufikia  14 mwaka huu  2020.

Bi .Adija alitaja sababu kubwa ya kupunguza wafanyakazi hao kuwa ni pamoja na  kupunguza  matumizi ya kampuni  kwa kipindi hiki ambacho  mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani katika mto Mkuju   bado hauja anza  kufanya kazi .

Hata  hivyo Adija  alifafanua sababu ya  kucheleweshwa  kwa uchimbaji wa  madini hayo kuwa ni kuporomoka  kwa  bei ya  madini hayo katika  soko la dunia ambako ndiko soko la madini hayo yanakouzwa.

Aidha  Adija  alisema licha ya  mradi wa kuchimba  madini katika mto Mkuju kutoanza rasmi  kampuni  ya Mantra Tanzania Limited inaendelea kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu ,afya na mazingira.

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo bwana  Peres  Kamugisha alimshukuru  Afisa uhusiano wa Mantra kwa kuendelea kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo  katika upande wa elimu afya na mazingira

Kamugisha  alitaja ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari  Nasuli pamoja na shule ya sekondari  Nangungu  kuwa ni jitihada ya kampuni hiyo  ambayo ilitoa fedha za kukamilisha ujenzi wa maabara katika shule hizo.

Naye mwalimu wa kitengo  cha walemavu katika  shule ya msingi  ufundi  Namtumbo bi.Bibiana  Adamu alisema  anamshukuru  afisa mahusiano wa kampuni ya Mantra kwa kukitembelea kitengo cha walemavu  kujionea changamoto na kuahidi  kuwasaidia  wanafunzi walemavu .

Kitengo cha walemavu katika shule ya ufundi Namtumbo kina jumla ya wanafunzi walemavu 44 ikiwa wasichana  11 na wavulana  33 huku  wenye matatizo  ya akili wasichana 7 wavulana  26 na viziwi wasichana  4 na wavulana 5 na waviungo wavulana 2.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake