ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 10, 2020
Urais 2020 waja na rekodi mpya
MWANDISHI WETU
WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikitarajia kufunga pazia wiki ijayo kwa wagombea kutoka vyama mbalimbali kuchukua fomu ya nafasi ya urais, idadi ya waliojitokeza kuwania nafasi hiyo hadi sasa inaelekea kuvunja rekodi ile ya mwaka 2015.
Hadi kufikia jana tayari wagombea nane kutoka vyama mbalimbali walikuwa wamefika NEC kuchukua fomu hizo, huku wengine wakitarajiwa kuchukua kesho na wiki ijayo.
Waliojitokeza kuchukua fomu hizo jana, ni mgombea wa nafasi ya urais, kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU) Mutamwega Magaiwa aliyekuwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Safia Berwa.
Mwingine aliyefika kuchukua fomu hiyo ni mgombea wa ACT, Wazalendo, Bernard Membe aliyekuwa ameongozana na mgombea mwenza wake pamoja na mgombea urais wa chama hicho upande wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.
Chama kingine kilichochukua fomu jana katika ofisi za NEC ni chama cha Alliance For Democratic Party (ADC) ambapo mgombea wa nafasi ya urais, Queen Sendiga naye aliambatana na mgombea mwenza wake, Shoka khamis Juma.
Chama kingine kilichochukua fomu jana ni Chama cha United Democratic Party (UPDP) ambapo mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho,Twalib Ibrahim Kadege alifika katika Ofisi za NEC akiwa na mgombea mwenza, Ramadhan Ally Abdallah.
Pazia la uchukuaji fomu za kugombea nafasi ya urais lilifunguliwa Jumatano, Agosti 5 mwaka huu ambapo mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wakulima(AAFP), Seif Maalim Seif alikuwa wa kwanza kufika katika ofisi hizo akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza wake Rashid Rai na baadhi ya wanachama wa chama hicho.
Mgombea wa pili aliyefika kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi hizo ni kutoka Chama cha Democratic Party(DP), Philipo Fumbo ambaye alitinga katika ofisi hizo saa 5:30 asubuhi akiwa peke yake bila mgombea mwenza, Zainab Juma Hamisi.
Mgombea wa tatu alikuwa kutoka Chama cha NRA, Leopard Mahona ambaye alifika katika ofisi hizo saa 6:30 mchana na mgombea mwenza wake, Hamis Ali Hassan.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alichukua fomu juzi katika Ofisi za NEC ambapo aliambatana na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa,Spika wa Bunge na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu,Dk.Bashiru Ally.
Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 waliojitokeza kuchukua fomu NEC kuwania urais waliokuwa ni wagombea nane tu.
Wagombea hao ni Anna Mghwira aliyegombea kupitia chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Chifu Lutalosa Yembe wa Alliance for Democratic Change (ADC), Edward Lowassa aliyegombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Katika orodha hiyo alikuwemo pia Fahmi Dovutwa wa chama cha United People Democratic Party (UPDP), Hashim Rungwe wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Janken Kasambala wa National Reconstruction Alliance (NRA).
Pia alikuwepo John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Machmillan Lyimo wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment