NA YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Kampuni ya Mantra Tanzania limited iliyotegemewa kuanzisha mgodi wa uchimbaji wa madini ya Urani katika kijiji cha Likuyusekamaganga wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma imepunguza wafanyakazi 70 kutokana na mgodi kutoanza kufanya kazi ya uchimbaji.
Akiongea akiwa shule ya Msingi Mwenge katika mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo Afisa Mahusiano wa kampuni ya Mantra Tanzania limited BI. Adija Pallangyo alisema Kampuni ya Mantra imepunguza wafanyakazi wake kutoka 84 mwaka 2014 na kufikia 14 mwaka huu 2020.
Bi .Adija alitaja sababu kubwa ya kupunguza wafanyakazi hao kuwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya kampuni kwa kipindi hiki ambacho mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani katika mto Mkuju bado hauja anza kufanya kazi .
Hata hivyo Adija alifafanua sababu ya kucheleweshwa kwa uchimbaji wa madini hayo kuwa ni kuporomoka kwa bei ya madini hayo katika soko la dunia ambako ndiko soko la madini hayo yanakouzwa.
Aidha Adija alisema licha ya mradi wa kuchimba madini katika mto Mkuju kutoanza rasmi kampuni ya Mantra Tanzania Limited inaendelea kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo katika sekta ya elimu ,afya na mazingira.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo bwana Peres Kamugisha alimshukuru Afisa uhusiano wa Mantra kwa kuendelea kushiriki kuchangia shughuli za maendeleo katika upande wa elimu afya na mazingira
Kamugisha alitaja ujenzi wa maabara katika shule ya sekondari Nasuli pamoja na shule ya sekondari Nangungu kuwa ni jitihada ya kampuni hiyo ambayo ilitoa fedha za kukamilisha ujenzi wa maabara katika shule hizo.
Naye mwalimu wa kitengo cha walemavu katika shule ya msingi ufundi Namtumbo bi.Bibiana Adamu alisema anamshukuru afisa mahusiano wa kampuni ya Mantra kwa kukitembelea kitengo cha walemavu kujionea changamoto na kuahidi kuwasaidia wanafunzi walemavu .
Kitengo cha walemavu katika shule ya ufundi Namtumbo kina jumla ya wanafunzi walemavu 44 ikiwa wasichana 11 na wavulana 33 huku wenye matatizo ya akili wasichana 7 wavulana 26 na viziwi wasichana 4 na wavulana 5 na waviungo wavulana 2.
No comments:
Post a Comment