ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 28, 2020

YANGA YAPATA KOCHA MPYA

By Mwandishi Wetu

KAMA ambavyo Mwanaspoti la leo Ijumaa lilivyoripoti juu ya Kocha Mkuu wa Yanga, kuwa ni Zlatko Krmpotic kutoka Serbia, Mkurugenzi wa Uwezeshaji wa GSM ambao ni wadhamini wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said amethibitisha ni kweli kocha huyo ndiye anayechukua nafasi ya Kaze Cedric.
Kaze alitangazwa kuchukua nafasi ya Luc Eymael aliyetimuliwa kwa ubaguzi wa rangi, lakini Mrundi huyo aliomba udhuru wa kupewa wiki tatu na mabosi wa Jangwani wakaamua kuachana naye na kumtafuta kocha mpya ambaye Mwanaspoti kupitia vyanzo vyake makini vilimtaja katika gazeti la leo kwa usahihi.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na kituo cha Wasafi FM asubuhi, Injinia Said alisema kocha huyo aliyewahi kuwapa ubingwa TP Mazembe ya DR Congo na Zesco United ya Zambia, ndiye Kocha Mkuu wa Yanga na anatarajiwa kutua Jumatatu kuja kuungana na Juma Mwambusi anayekuwa Kocha Msaidizi baada kuingia naye mkataba wa mwaka mmoja.

"Ni kweli Kocha Mkuu mpya ni Zlatko Krmpotic ambaye anatarajiwa kuingia nchini na nikiri kama kuna jambo lililokuwa jepesi basi ilikuwa kwenye uteuzi wa kocha huyo, kwani tayari jina lake lilikuwa kati ya waombaji 21, akiwamo mzawa mmoja aliyekuwa akiomba Kocha msaidizi," alisema Injinia Hersi.

Alipoulizwa juu ya kuridhia kufanya kazi na wasaidizi anaowakuta ambao lilikuwa pendekezo la Kaze, Injinia huyo alisema alifahamishwa na kuridhia na wanaimani ataifikisha Yanga pale wanapopataka.
Mwanaspoti lililokuwa la kwanza pia kuripoti juu ya ujio wa Kaze na uteuzi wa Mwambusi kama Kocha Msaidizi, limeandika wasifu wa kocha huyo na mafanikio yake.
Kwa taarifa zaidi juu ya kocha huyo na mipango mingine ya kuelekea Siku ya Kilele cha Wiki ya Mwananchi, endelea kufuata mitandao ya kijamii ya Mwananchi na kulisoma Mwanaspoti la kesho kwa utamu zaidi.

No comments: