Tuesday, September 15, 2020

Chadema yadai kuhujumiwa na NEC

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iharakishe kupitia rufaa za ubunge na udiwani ili wagombea wa chama hicho waweze kupata haki na kuanza kampeni. PICHA: SILVAN KIWALE

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimedai kuwa kinahujumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), hivyo kimeiandikia barua ili iainishe rufaa za wagombea ubunge na udiwani zilizotolewa na kufanyiwa uamuzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Chadema, John Mnyika pamoja na mambo mengine alisema katika barua hiyo pia wameitaka NEC kuwachukulia hatua wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo kwa kuwaengua wagombea wao bila kufuata taratibu.

“Inasikitisha tangu kampeni zianze ni siku 18 sasa, lakini bado tume haijamaliza uamuzi kuhusu rufaa za wagombea ubunge na udiwani.

“Bado kuna rufaa 20 ambazo wabunge wetu wameenguliwa, kwa taarifa ambazo tunazo ndani ya tume tayari uchambuzi kuhusu rufaa zote ziko tayari, lakini kuna mchezo unafanywa pale tume kuchelewesha ili kuwachelewesha wagombea wetu kuanza kampeni mapema.

“Sasa kutokana na hujuma hizi, leo (jana) nimemwandikia mkurugenzi wa NEC ili wawarejeshe wagombea wetu wote waliokata rufaa katika mchakato wa uchaguzi.

“Kinachoonekana kwa tume kutoa taarifa kidogo kidogo inafanya kupoza hasira za umma kuwa wanashughulikia, pamoja na barua hii tuliyoiandikia tume na kwa kuwa kesho (leo) ni siku ya demokrasia duniani, wadau wote wa demokrasia tuungane kwa kuwa demokrasia yetu hapa nchini iko shakani juu ya tume kutokuwa huru,” alisema Mnyika.

Aidha alisema jumla ya rufaa 18 ambazo wagombea wao wa ubunge wamerejeshwa, lakini tume haijawapa barua rasmi ya maandishi kuhusu uamuzi huo.

Mnyika alisema anatoa salamu kwa wagombea ubunge wa CCM waliopita bila kupingwa kuwa watambue kuwa kubebwa kwao na tume si mwisho wa mchakato wao wa kudai haki.

“Natoa salamu kwa wagombea ubunge wa CCM waliopita bila kupingwa wakiongozwa na Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), kuwa sio mwisho wa mchakato wetu wa kudai haki, tunawataka wanachama wetu na wananchi kukishauri chama chetu hatua za kuchukua, hivyo Majaliwa na wenzake wasidhani tume imewabeba kwa mbeleko basi wako salama,” alisema Mnyika.

Katika hilo, alisema hawatafumbia macho hujuma za wazi za kuwanyima wananchi ridhaa ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Alitaja baadhi ya majimbo ambayo wagombea wake hadi sasa uamuzi wa rufaa haujatolewa ni pamoja na Butiama, Handeni Vijijini, Kavuu, Kwimba, Kondoa Vijijini, Gairo, Morogoro Mjini, Songwe, Ludewa, Msalala na Lupa.

“Chadema imekata rufaa zaidi ya 400 za udiwani, lakini mpaka sasa ni rufaa 100 tu ambazo zimetolewa maamuzi suala ambalo linaminya demokrasia, kwa mfano Jimbo la Ukerewe msimamizi wa uchaguzi ameanza kuengua wagombea wa udiwani ambao hawakuwekewa pingamizi,” alisema Mnyika.

Kutokana na maamuzi hayo yaliyofanywa na msimamizi wa Jimbo la Ukerewe, Mnyika alisema Chadema imeiomba tume kuchukua hatua stahiki.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa NEC, Dk. Wilson Mahera alikiri kupokea barua hiyo ya Chadema huku akisisitiza kuwa taarifa kwamba chama hicho kinahujumiwa si za kweli.

“Ni kweli barua yao nimepokea jana (juzi). Lakini ni waongo na waache uongo… hata sasa unaweza kuja hapa jengo la Mwalimu Nyerere Dar es Salaam, tuko kwenye kikao tunaendelea kupitia hizo rufaa.

“Waache kutusumbua, sasa wao wanapiga kelele tungetoa hizo rufaa haraka hata hao wabunge wao wasingerudi, waache uzandiki, upuuzi na uongo.

“Wanapenda sana kulalamika, afadhali hata mnatuuliza hayo… hapa tunaangalia vielelezo lakini wao wanaleta nongwa, waache kabisa,” alisema Dk. Mahera.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake