Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye (Wa nne kulia) wakizindua jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma jana. Wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma jana. Baadhi ya Viongozi wa Serikali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Kigoma. Wa kwanza kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. George Simbachawene akifuatiwa na Waziri wa Elimu Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye.Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma.
Na Lydia Churi-Mahakama, Kigoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Mahakama ya Tanzania kutumia miundombinu iliyojengwa ili kuimarisha huduma za utoaji haki nchini.
Akizindua jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma pamoja na Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye leo, Rais Magufuli amesema haitakuwa na maana kwa Mahakama kujenga majengo mazuri kama wananchi watanyimwa haki zao kwa sababu ya rushwa na vitendo vingine vya ukosefu wa maadili.
“Natoa wito kwa Majaji kuhakikisha Mahakama hii inatimiza malengo ya kujengwa kwake kwa kutokuwa na mlundikano wa mashauri”, alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia alitoa wito kwa Watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania kuitunza miundombinu ya majengo yanayojengwa ili yadumu na kurahisisha suala zima la utoaji haki nchini.
Akielezea kujengwa kwa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Kigoma kutasaidia kupunguza ucheleweshwaji wa mashauri mahakamani na kupunguza gharama walizokuwa wakitumia wananchi kufuata huduma za Mahakama Kuu umbali wa kilometa 430 mkoani Tabora.
Aidha, Rais Magufuli amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na viongozi wote wa Mahakama kwa kujenga jengo la kisasa la Mahakama Kuu kanda ya Kigoma. Alisema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2016/17 hadi 2021-22.
Rais alisema mbali na Mahakama iliyozinduliwa, katika kipindi ch miaka mitano, Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu kanda ya Musoma na kufanya ukarabati na upanuzi wa jingo la Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga. Majengo mengine yaliyojengwa ni Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa mipya ya Geita, Simiyu na Manyara pamoja na Mahakama za wilaya za Kilwa, Ruangwa, Kondoa, Longido, Bukombe, na Mahakama kadhaa za Mwanzo.
Akizungumzia uteuzi wa Majaji, Rais Magufuli kati yam waka 2015 na sasa jumla ya Majaji 50 waliteuliwa wakiwemo 11 wa Mahakama ya Rufani na 39 wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Aliongeza kuwa Mahakimu 396 waliajiriwa katika kipindi hicho na hivyo kuongeza idadi ya Mahakimu kutoka 700 na kufikia 938.
Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye akizungumza wakati wa hafla hiyo aliishukuru Tanzania kwa jitihada zake za kurejesha Amani nchini Burundi.
“Tanzania ilikubali kubeba Msalaba wa nchi ya Burundi na kukubali kutunza raia wa Burundi kama wakimbizi nchini”, alisema na kuongeza kuwa amefika nchini Tanzania ili kushukuru Serikali kwa jitihada zake ilizozifanya.
Naye Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama kutoa huduma bora zinazoendana na hadhi ya nchi yenye kipato cha Kati.
“Ubora wa huduma ya utoaji haki hautegemei jengo zuri peke yake, watumishi waadilifu na wanaofanya kwa bidii, umakini na weledi ndio watawezesha jengo hili zuri liheshimiwe na wananchi”, alisema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, baada ya Benki ya Dunia kuitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za uchumi wa kipato cha kati watumishi wa Mahakama wanapaswa kukumbuka kuwa uchumi wa kipato cha kati ni suala linalohusu pia ubora wa huduma kwa umma.
“Huduma zetu Mahakama hatuna budi kulingana au kuzidi hadhi ya uchumi wa nchi zenye kipato cha kati.
Jaji Mkuu amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwa kupata jengo lililosogeza huduma za Mahakama Kuu na pia kuwezesha kuanza kwa huduma za Mahakama ya Rufani kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali No. 579 la tarehe 24/7/2020, kutangazwa kuwa Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufani.
Alisema uwepo wa jengo la Mahakama Kuu Kigoma ni matunda ya ushirikiano baina ya Serikali na Mhimili wa Mahakama katika kuiwezesha Mahakama kuwa na miundombinu ya Majengo ya kisasa.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake