Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwasalimia wananchi waliofika kumpokea Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Rais wa Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye akizungumza na Wananchi katika uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
NA JOHN BUKUKU-KIGOMA
Dk.Magufuli amesema katika mazungumzo yao na Mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Mh. Evariste Ndayishimiye pamoja na mambo mengine wamezungumzia madini ya Nicol ambayo yapo katika eneo Msangati nchini Burundi na kwa upande wa Tanzania yapo eneo la Kabanga.
Katika eneo hili la madini ya Nicol wamekubaliana kushirikiana hasa kwa sababu tayari Tanzania imeshaanzisha maduka ya kununua madini na pia wamekubaliana kujenga kiwanda cha kuchenjua madini ya Nicol ili kuyaongezea thamani na kisha kuyauza na kupata fedha ili kukuza uchumiwa nchi zao..
Rais Dk John Pombe Magufuli ameyasema hayo wakati marais hao wakitoa taarifa ya pamoja mara baada ya mazungumzo yao kumalizika kwenye Ikulu Ndogo ya Mjini Kigoma mkoani humo.
Rais Magufuli amesema Rais Ndayishimiye amechagua Tanzania kuwa nchi yake ya kwanza mara tu baada ya kuchaguliwa, ameonesha heshima kubwa lakini inaonesha ni jinsi gani Tanzania na Burundi wamekuwa ndugu.
Katika mazungumzo hayo Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DK.John Magufuli na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Evarist Ndayishimiye wamekubaliana mambo sita kwa ajili ya kuleta maendeleo katika nchi zao.
Rais wa Burundi Evarist Ndayishimiye kwa upande wake amesema mambo hayo ni miundombinu kama Reli, Barabara, Madini, Ufugaji, Usafiri wa majini, Biashara, pamoja na ulinzi na usalama.
Rais Ndayishimiye amesema wamekubaliana kuimarisha miundombinu ya barabara, reli pamoja na bandari ambapo katika eneo la reli wataunganisha reli kutoka Uvinza , Msongati hadi Gitega nchini Burundi yenye urefu wa kilometa 200.
“Eneo la kibiashara bado nchi zetu hazijatumia vizuri fursa zilizopo kwa kila nchi, hivyo tumekubaliana kuendelea kudumisha biashara na kwa ngazi ya kikanda tumezungumzia hali ya usalama katika maeneo ya maziwa makuu ambapo tumekubaliana kudumisha umoja” Amesema Mh. Ndayishimiye
Aidha amesema kuwa wamejadiliana kwa kina kuhusu masuala ya kisiasa , kiuchumi na kiutamaduni na wamekubaliana kuendeleza biashara ya madini na katika kufanikisha hilo wamekubaliana mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote mbili kuitisha mkutano mapema kujadili masuala hayo.
Kwa upande wa kimataifa Rais Ndayishimiye amesema wamekubaliana kukumbushana ajenda ya Afrika kuhusu maendeleo lakini pia kuhusu wakimbizi, amesema hivi sasa wakimbizi wengi wanarudi Burundi kwani hali ya amani na usalama imeimarika zaidi ukilinganisha na kipindi kilichopita.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake