WATU wawili waliobaka watoto, wamekiona cha moto baada ya mahakama kwa nyakati tofauti, kuwahukumu kifungo cha maisha jela. Wa kwanza kupewa hukumu hiyo na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Singida, ni Hussein Aziz ambaye alikiri kosa la kumlawiti mtoto wa miaka minne (Jina linahifadhiwa).
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Robert Oguda alisema anatoa adhabu kali kwa mshtakiwa, ili iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hiyo.
Awali, Mwanasheria wa Serikali, Elizaberth Barabara alisema kwamba, mshtakiwa alitenda kosa hilo la kumlawiti mtoto huyo mwenye umri wa miaka minne Agosti 6 mwaka huu, katika Mtaa wa Minga mjini Singida.
Mwanasheria huyo alidai kuwa, watoto walimfuata hadi alipokuwa anachunga ng’ombe, ambako alitenda kosa hilo na kwamba, hakuwa amefanya tendo hilo mara moja, bali alikuwa akifanya mara kwa mara kwa mtoto huyo.
Mwanasheria Barabara alisema, mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yake, alikiri kwa kusema kwamba, hakuwa akifanya kitendo hicho kwa mtoto huyo peke yake, bali kulikuwa na mtu mwingine ambaye naye alikuwa akimfanyia kitendo hicho bila kugundulika. Baada ya kusomewa shtaka hilo na kukiri, kabla ya kutiwa hatiani, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na akawa na haya ya kusema.
“Ni kweli nilifanya kitendo hicho, hivyo naomba msamaha na naahidi kwamba, sitarudia tena kufanya kitendo kama hicho,” alisema Aziz. Pia katika utetezi wake, Aziz alikiri kwamba, kitendo alichokifanya kwa mtoto huyo hakikuwa kizuri, hivyo aliiomba mahakama imuonee huruma na kumpa adhabu ndogo.
Hakimu Oguta alimhukumu kifungo cha maisha jela, ili iwe fundisho kwa wengine wanaokusudia kutenda kosa kama hilo. Wakati hayo yakitokea, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya, Katoki Mwakitalu naye amemhukumu, Venas Edward (48), kutumikia kifungo cha maisha kwa kosa la kumnajisi mtoto wa kike wa miaka nane.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Katoki Mwakitalu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo alisema, upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi wanne na kielelezo kimoja, ambacho ni hati ya kutibiwa (PF3) na kuthibitisha kutenda kosa hilo bila shaka yoyote.
Ilielezwa mahakamani hapo kuwa, mtoto huyo (jina linahifadhiwa) alipelekwa kwa Venas ili amtibu kwa dawa za mitishamba, badala yake akamnajisi kwa kutumia ujanja wa kumtuma mama yake dukani na aliporudi alimkuta mtoto akilia, na alipomhoji aligundua ana maumivu sehemu za siri alizomharibu mtu huyo.
Mama wa mtoto huyo alisema, alipombana mtoto wake kwa kumuuliza ni nani aliyemfanyia kitendo hicho, ndipo alimjibu kuwa ni mshtakiwa kamfanyia kitendo hicho kibaya. Hakimu Mwakitalu alisema, anamhukumu mtuhumiwa kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa wengine.
STORI ELVAN STAMBULI, Risasi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake