WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewakumbusha wauguzi wote nchini kuhakikisha wanajiendeleza kielimu, ili baadae wawe na maarifa zaidi ambayo yatawaongezea ubunifu na utendaji wao wa kazi.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ziada Sellah, kwenye mkutano baina yake na wauguzi na wakunga wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida.
Mkurugenzi huyo licha ya kusisitiza umuhimu wa kujiendeleza kielimu, pia amewapongeza watumishi wa kada ya uuguzi mkoani Singida, kwa kutekeleza vema majukumu yao, licha ya kukabiliana na changamoto mbalimbali wakiwa kazini.
“Niwapongeze wauguzi wote kwa jitihada zenu mnazofanya kila siku za kuwahudumia wananchi,mmekua muda mwingi mko na wagonjwa na hamchoki kutoa huduma kwa rika zote”Alisema Bi. Sellah
Alisema Wizara ya Afya inatoa udhamini kwa masomo ya ngazi za juu kwa watumishi wa sekta ya afya kila mwaka,hivyo wanapaswa kuomba nafasi hizo bila kusita.
Naye Muuguzi mkuu wa mkoa wa SINGIDA Hyasinta Alute, amesema kuwa hospitali na vituo vingi vya afya mkoani humo havina magari ya kubebea wagonjwa, hali inayohatarisha maisha ya wajawazito wanaopata rufaa, huku muuguzi mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Theresia Ntui, akiwaasa wauguzi kufanya kazi kwa weledi ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaofika Hospitalini hapo kupata huduma.
No comments:
Post a Comment