Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba akihutubia wakazi wa Njombe leo alipofungua Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kitaifa na kubainisha kuwa Taifa lina utoshelevu wa chakula wa asilimia 124.
Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba (katikati) akitazama bidhaa za wajasiliamali wanaoongeza thamani mazao ya kilimo. Kulia kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah na kushoto ni Afisa Kilimo Wilaya ya Njombe Eritha Mligo.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usalama wa Chakula Dkt.Honest Kessy akitoa salamu za wizara kwa niaba ya Katibu Mkuu Kilimo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa mkoani Njombe.
Sehemu ya wananchi wa Njombe wakifuatilia matukio wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kitaifa mkoani Njombe leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dtk.Rashid Tamatamah akitoa salamu za wizara yake wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani kitaifa mkoani Njombe leo.Naibu Waziri Kilimo Omary Mgumba (kushoto) akipata maelezo kuhusu lishe bora kupitia ‘ Piramidi la Chakula” toka kwa Maria Ngilisho Afisa Mtafiti Mwandamizi(kulia) wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini.
( Habari na picha na Wizara ya Kilimo)
Serikali ya awamu ya tano imefanikiwa kutumia shilingi Bilioni 56 kujenga vihenge vya kisasa na maghala ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka kufikia tani 501,000 mwaka 2020 toka tani 250,000 mwaka 2015.
Mafanikio hayo ya serikali yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba leo (10.10.2020) wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kitaifa mkoani Njombe.
Mgumba amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeweza kusimamia na kutekeleza vyema ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 na kuiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula kwa kujenga vihenge vya kisasa na maghala.
“ Serikali imetumia Shilingi Bilioni 56 kujenga vihenge vya kisasa na maghala katika kanda nane (8) za NFRA ambapo uwezo wa kuhifadhi utaongezeka toka tani 250,000 mwaka 2015 hadi tani 501,000 mwaka 2020)” alisema Mgumba.
Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani Naibu Waziri Mgumba alisema Taifa lipo katika hali ya usalama kutokana na uwepo wa utoshelevu wa chakula kufuatia juhudi za wakulima, wafugaji na wavuvi.
“Kwa mujibu wa takwimu za uzalishaji na tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya msimu wa 2019/2020, inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula unatarajia kufikia tani 17,742,388 ambapo mahitaji ni tani 14,347,955” alisema Naibu Waziri Mgumba.
Naibu Waziri huyo alibainisha kuwa mahitaji yakilinganishwa na uzalishaji nchi inategemewa kuwa na ziada ya tani 3, 511,620 za chakula ambapo tani 1,322,020 ni za mazao ya nafaka na tani 2,072,413 ni za mazao yasiyo nafaka.
Kauli mbiu ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu inasema ‘Kesho Njema Inajengwa na Lishe Bora Endelevu’ ambapo Serikali imedhamiria kutatua changamoto za lishe kwa kuendelea kutekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe (National Multsectoral Nutrition Action Plan- 2016/2017- 2020/2021) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDPII) alisisitiza Mgumba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhandisi Marwa Rubirya alisema mkoa wake una ziada ya chakula tani 700,000 lakini wanakabiliwa na tatizo la udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano unaofikia asilimia 49.4 mwaka 2019.
Alibainisha kuwa mkoa wake kupitia maadhimisho haya utaweza kufikisha elimu ya lishe bora kwa wananchi ili kuwa na nguvu kazi yenye afya bora kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.
“Tumepanga kama mkoa kupambana na tatizo la udumavu kwa watoto ili tufikie angalau asilimia 33 toka 49.4 ya sasa kwani Njombe ina vyakula vingi isipokuwa hatuli vema” alisisitiza Mhadisi Marwa .
Mhandisi Marwa alibainisha kuwa mkoa wa Njombe unahitaji wawekezaji wengi kwenye sekta za kilimo,mifugo na uvuvi kutokana na uwepo wa ardhi yenye rutuba na hali ya hewa nzuri.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Rashid Tamatamah alisema sekta hiyo imeendelea kukua na kuchangia asilimia 30 ya protini inayotokana na wanyama na inatoa ajira kwa Watanzania takribani milioni 4.5.
Dkt.Tamatamah aliongeza kuwa katika mwaka 2019/20, Sekta ya Uvuvi ilikua kwa kiwango cha asilimia 1.5 na kuchangia Pato la Taifa (GDP) kwa asilimia 1.71 ambapo uzalishaji wa samaki kutoka maji ya asili kwa mwaka 2019/20 ulifikia takribani tani 497,567 na katika uzalishaji wa mazao ya viumbe maji kufikia tani 18,716.56.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yamezinduliwa leo mkoani Njombe na yatafikia kilele tarehe 16 mwezi huu kwa lengo la Kutathmini hali ya chakula nchini na nje ya nchi na kuhamasisha uzalishaji na upatikanaji wa chakula bora, salama na cha kutosha kuanzia ngazi ya Kaya, Wilaya, Mkoa, Taifa na ki-Mataifa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake