Monday, October 12, 2020

UFAFANUZI KUHUSU UPOTOSHAJI JUU YA UCHAPISHAJI WA KARATASI ZA KUPIGIA KURA KWENYE UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2020

Dodoma,

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imebaini kuwepo kwa taarifa ya upotoshaji kuhusu mchakato wa zabuni ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 na jina la Mzabuni aliyeshinda zabuni hiyo. Taarifa hiyo potofu iliyonukuliwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii imetolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Bw. John Mnyika wakati alipokuwa akiongea na vyombo habari.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi, kwa mujibu wa Ibara ya 74(6)(b) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imepewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa upande wa Tanzania bara. Ili iweze kutekeleza jukumu hilo, Tume imeweka mipango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba vifaa vya uchaguzi vinapatikana mapema, vinahifadhiwa vizuri, vinafungashwa kulingana na uhitaji na vinasafirishwa katika hali ya usalama hadi kwenye vituo vya kupigia kura.

Katika kufanikisha azma hiyo, Tume iliandaa mpango wa manunuzi wa vifaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa mujibu wa Kifungu cha 49 (2) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura ya 410 ikisomwa kwa pamoja na kanuni kwenye GN 446 ya mwaka 2013.

Tangazo la fursa za zabuni la ujumla (General Procurement Notice) liliwekwa kwenye tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) tarehe 2 Julai, 2019 na kurudiwa tena tarehe 13 Disemba, 2019 likiwa katika mfumo wa TANEPS. Vile vile, Tume ilitangaza kwenye Gazeti la Serikali la Daily News la tarehe 8 Julai 2019 kwa ajili ya kuufahamisha umma kuhusu fursa za Zabuni zitakazotangazwa baadae na Tume. Umma uliofahamishwa ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa wakiweno wale wa chama cha CHADEMA.

Katika mpango huo wa Manunuzi jumla ya zabuni 47 ziliorodheshwa ikiwemo zabuni Na. IE/018/2019-20/HQ/G/GE/13 iliyohusu Uchapishaji wa Karatasi za kupigia Kura. Njia ya kumpata mshindi iliyotangazwa ni ya ushindani wa wazi wa kimataifa (International Competetive tender). Hivyo, zabuni hiyo ilitangazwa na PPRA tarehe 09 Machi, 2020 kwenye mtandao wa TANEPS, ikarudiwa kutangazwa na Tume kwenye Gazeti la Daily News la tarehe 10 Machi, 2020 na baadae gazeti la kimataifa la The East African la tarehe 14 Machi, 2020. Ufunguzi wa zabuni hiyo ulifanyika tarehe 08 April, 2020 na jumla ya makampuni yaliyoshiriki yalikuwa ni matatu (3), yote yalitoka nje ya nchi kama ifuatavyo:
1. M/s Ren-Form CC ya Afrika Kusini 2. M/s Ellams Products Limited ya Kenya 3. M/s Al Ghurair Printing and Publishing LLC ya Dubai

Baada zabuni kufunguliwa na kufanyiwa uchambuzi, Mzabuni M/s Ren-Form CC wa Africa Kusini alitangazwa na Mamlaka husika (PPRA) kuwa mshindi. Hivyo, mzabuni aliyetajwa kwenye taarifa za uzushi kwa jina la Jamana Printers hakuhusika popote kwenye mchakato huo.

Taarifa hiyo potofu imenukuliwa pia ikituhumu Tume kwamba haikutoa taarifa kwa umma kuhusu mshindi wa zabuni ya karatasi za kupiga kura. Tume inapenda kufafanua kuwa wajibu na mamlaka ya kutangaza washindi wa zabuni za umma kwa mujibu wa Kanuni ya 235 na 236 za GN 446 ya mwaka 2013 iliyoandaliwa chini nya sheria ya Manunuzi umma, Sura ya 410 ni wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), ambayo huyaweka matokeo yote wazi ya washindi wa zabuni kwenye Tender portal inayopatikana kwenye tovuti yake www.ppra.go.tz na jarida lake (Tanzania Procurement Journal). PPRA ilifanya hivyo, na mshindi wa zabuni hiyo alitangazwa kwenye Tender portal na jarida hilo ambalo lipo wazi wakati wote kwa umma.

Taarifa hiyo potofu pia iliishutumu Tume kutoishirikisha Kamati ya Kitaifa ya Manunuzi na Lojistiksi ambayo inajumuisha wajumbe kutoka vyama vya siasa katika hatua zote za manunuzi ya vifaa vya uchaguzi. Tume inapenda umma ufahamu kwamba michakato ya Manunuzi ya umma inasimamiwa na sheria ya manunuzi ya Umma, Sura ya 410, ambayo haitoi nafasi kabisa kwa kamati nyingine yoyote

zaidi ya Bodi ya Zabuni ya Tume kusimamia michakato ya manunuzi kuanzia kuitisha zabuni, kupokea zabuni na kuzifungua, kufanya uchambuzi na kuidhinisha mshindi. Hivyo kamati ya manunuzi na lojistiksi ya kitaifa inahusishwa tu chini ya dhana ya uwazi na ushirikishwaji ambapo inaweza pale inapobidi kutoa maoni na ushauri kwa Tume.

Pamoja na nia njema ya Tume kuvishirikisha vyama vya siasa kwenye eneo la upatikanaji wa vifaa vya uchaguzi kwa ajili ya kupokea ushauri wao, vyama vingi kikiwemo chama cha CHADEMA havikuteua majina ya wajumbe wa kuunda kamati ya kitaifa ya Manunuzi na Lojistiksi licha ya vyama hivyo kuandikiwa barua na Tume ya tarehe 30 Juni, 2020. Hadi siku ya kikao cha kwanza cha kamati hiyo kilichofanyika tarehe 8 Oktoba 2020 chama cha CHADEMA na baadhi ya vyama vingine vilikuwa havijateua na kuwasilisha kwenye Tume majina ya wawakilishi wa kuunda kamati hiyo ya kitaifa. Mwenendo huu wa vyama vya siasa umesababisha kuchelewa kuanza kwa wakati shughuli za kamati hii

Tume inawataka wananchi kuipuuza taarifa hiyo potofu ambayo inalenga kuleta taharuki kwa jamii. Aidha, Tume inapenda kutumia fursa hii kuwahakikishia wananchi kwamba maandalizi yote ya uchaguzi mkuu wa 2020 yahusuyo vifaa yamekamilika na kwa sasa kazi inayoendelea kupokea na kupeleka vifaa hivyo kwenye majimbo ya uchaguzi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavishauri vyama vya siasa katika kipindi hiki cha kampeni vielezee sera za vyama vyao na kuwanadi wagombea wao badala ya kujikita katika kueneza taarifa za uzushi.

Imetolewa na:

Darles

Dkt. Wilson M. Charles MKURUGENZI WA UCHAGUZI TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI 

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake